MCAs wakabiliana wakijadili mswada wa BBI

Na WAANDISHI WETU

FUJO zilizuka Alhamisi kwenye Bunge la Kaunti ya Baringo, madiwani waliporushiana makonde kutokana na mzozo kuhusu mswada wa BBI.

Jijini Nairobi, sekretariati inayosimamia mchakato wa marekebisho ya katiba kupitia BBI ilieleza matumaini ya mswada huo kupitishwa na mabunge 35.

Mswada huo ambao tayari umepitishwa na mabunge matatu, umewasilishwa mbele ya mabunge 22.

Mwenyekiti mwenza wa asasi hiyo, Bw Dennis Waweru, alisema wana matumaini kwamba mabunge 24 yanayohitajika yatapitisha mswada huo kufikia mwisho wa mwezi huu.

Alhamisi, Homa Bay ilikuwa kaunti ya tatu kuupitisha baada ya Siaya na Kisumu. Mswada huo umeshawasilishwa mbele ya mabunge ya Murang’a, West Pokot, Kajiado, Vihiga, Busia, Embu, Laikipia, Meru, Nakuru, Nyandarua, Nyeri, Tharaka Nithi, Nairobi, Kirinyaga, Makueni, Machakos, Kiambu, Kitui na Baringo.

Kwenye kisa cha Baringo kilichodumu kwa karibu nusu saa, kizaazaa hicho kilianza MCA Ernest Kibet alipodai kupigwa makonde mgongoni na mwenzake wa Mogotip, Bw Charles Kosgei.

MCA wa chama cha Kanu ambao ni wachache, walidai wakikuwa wakidharauliwa na wenzao wa Jubilee, huku Amaya Selemoi akidai kulikuwa na njama ya kuuangusha mswada huo.

“Bw Spika, najua kuna baadhi ya wanachama wa Jubilee wanaopanga kuuangusha mswada huu wa serikali. Hii si sawa. Huu mswada wa BBI ni kama Mungu aliona mateso yetu na ameuleta kutuokoa,” akasema.

Katika bunge la Homa Bay, madiwani wote walipitisha mswada huo bila kupingwa, muda mfupi baada ya kuwasilishwa na mwenyekiti wa kamati ya haki na sheria Agimba Ayieta aliyeungwa na diwani maalumu, Kevien Onyango.

Spika Elizabeth Ayoo aliyeongoza kikao cha kwanza cha bunge hilo baada ya likizo alitaja tukio hilo kuwa ya kihistoria. Madiwani walikuwa tayari kupitisha mswada huo wakitaja manufaa ambayo watapata hasa ya kifedha kama vile kuanzishwa kwa hazina ya wadi. Hata mvua na baridi kali haikuwazuia kufika mapema kujadili na kupitisha mswada huo.

PATRICK LANG’AT na GEORGE ODIWUOR

Habari zinazohusiana na hii

BBI YAINGIA ICU

Kwani kuliendaje?