• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Manchester City wakomoa Spurs na kuendeleza ubabe wao katika EPL

Manchester City wakomoa Spurs na kuendeleza ubabe wao katika EPL

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City waliendeleza ubabe wao katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumamosi kwa kuwapiga Tottenham Hotspur 3-0 katika mechi iliyowapa ushindi wa 15 mfululizo.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City walifungua pengo la alama saba kileleni mwa jedwali la EPL na sasa wanajivunia pointi 53 huku Leicester City wakiwa na alama 46 baada ya kutoka nyuma na kuwapepeta mabingwa watetezi Liverpool 3-1.

Kiungo Ilkay Gundogan aliwafungia Man-City mabao mawili katika dakika za 50 na 66 baada ya Rodri kuwafungulia waajiri wake hao karamu ya mabao kupitia penalti ya dakika ya 23.

Nusura Raheem Sterling awafungie Man-City bao la nne mwishoni mwa kipindi cha pili ila kombora lake likadhibitiwa vilivyo na kipa Hugo Lloris. Afueni kubwa zaidi kwa Man-City ni kwamba wangali na mchuano mmoja zaidi wa kusakata ambao huenda ukawapa fursa ya kufungua mwanya wa alama 10 kati yao na Leicester iwapo watawatandika Everton mnamo Februari 17, 2021 ugani Goodison Park

Wachezaji wa Tottenham na kocha wao Jose Mourinho waliondoka uwanjani wakiinamisha vichwa kwa aibu ya kupepetwa ugani Etihad.

Waliposhinda mchuano wa mkondo wa kwanza wa EPL uliowakutanisha na Man-City mnamo Novemba 2020, Tottenham walipaa hadi kileleni mwa jedwali.

Tangu wakati huo, Man-City wamejizolea alama 41 kutokana na 45 ambazo walikuwa na uwezo wa kutia kapuni na ushindi dhidi ya Tottenham uliwaweka pazuri zaidi kutawazwa mabingwa wa EPL msimu huu.

Kwa upande wao, Tottenham wamejikusanyia alama 16 pekee kutokana na mechi 14 zilizopita na wamepoteza michuano minne kati ya tano za awali katika mashindano yote. Kichapo kutoka kwa Man-City kiliwasaza Tottenham katika nafasi ya tisa kwa alama 36 sawa na Aston Villa walioambulia sare tasa dhidi ya Brighton katika mechi nyingine ya EPL mnamo Jumamosi usiku.

Ilivyo, huenda ikawa vigumu zaidi kwa Mourinho kumzidi maarifa mshindani wake Guardiola wakati Man-City na Tottenham watakaposhuka dimbani kuwania ubingwa wa Carabao Cup kwenye fainali ya mwaka huu 2021 itakayochezewa ugani Wembley mnamo Aprili 25.

Isipokuwa mpira wa ikabu alioelekezewa na Harry Kane mwanzoni mwa kipindi cha kwanza, kipa Ederson Moraes hakuwa na kazi kubwa ya kufanya katikati ya michuma ya Man-City hadi fowadi Erik Lamela alipomwelekezea fataki nyingine aliyoidhibiti kirahisi katika dakika ya 58.

Mabao mawili yalifungwa na Gundogan kwenye mechi hiyo yalifikisha idadi ya magoli yake hadi 11 kutokana na mechi 12 za hadi kufikia sasa msimu huu. Hata hivyo, aliondolewa uwanjani mwishoni mwa kipindi cha pili kwa kile ambacho Guardiola alisisitiza ni jeraha la paja ambalo huenda likamweka nje kiungo huyo raia wa Ujerumani kwa wiki tatu zijazo.

Man-City ndicho kikosi cha kwanza cha EPL kutofungwa bao katika mechi 14 kutokana na 23 za ufunguzi wa msimu wa EPL tangu Man-United (17) na Chelsdea (14) mnamo 2008-09.

Man-City kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Everton mnamo Jumatano huku Tottenham wakirejelea kampeni zao za Europa League katika hatua ya 32-bora dhidi ya Wolfsberger ya Austria mnamo Alhamisi ya Februari 18, 2021, jijini Budapest, Hungary.

MATOKEO YA EPL (Februari 13):

Leicester 3-1 Liverpool

Palace 0-3 Burnley

Man-City 3-0 Tottenham

Brighton 0-0 Aston Villa

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Uganda yarukia EU kwa kutaka iwekewe vikwazo

Napoli wazamisha Juventus kwenye Serie A na kuokoa kazi ya...