• Nairobi
  • Last Updated December 2nd, 2023 3:45 PM
Napoli wazamisha Juventus kwenye Serie A na kuokoa kazi ya kocha Gattuso

Napoli wazamisha Juventus kwenye Serie A na kuokoa kazi ya kocha Gattuso

Na MASHIRIKA

NAPOLI walimpunguzia kocha wao Gennaro Gattuso presha ya kupigwa kalamu kwa kuwapiga Juventus katika ushindi wa 1-0 uliopiga breki kasi ya kujifufua kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo Jumamosi usiku.

Bao la pekee na la ushindi kwa upande wa Napoli lilijazwa kimiani kupitia penalti ya Lorenzo Insigne katika dakika ya 31. Penalti hiyo ilitokana na tukio la nahodha wa Juventus, Giorgio Chiellini aliyekuwa akisakata mchuano wake wa 400 katika Serie A kuunawa mpira ndani ya kijisanduku.

Bao la Alvaro Morata ambalo vinginevyo lingesawazisha mambo mwishoni mwa kipindi cha pili lilikataliwa na refa kwa kuwa lilifungwa wakati ambapo Chiellini alikuwa ameotea.

Kipa Alex Meret wa Napoli alifanya kazi ya ziada katika vipindi vyote viwili vya mchezo kwa kupangua makombora mazito aliyoelekezewa na masogora wa Juventus wakiwemo Federico Chiesa, Morata na Cristiano Ronaldo aliyepoteza nafasi kadhaa za wazi.

Kabla ya kutandazwa kwa mchuano huo, vyombo vingi vya habari nchini Italia vilikuwa vimesisitiza kwamba Gattuso angalitimuliwa na waajiri wake iwapo Napoli wangalizidiwa maarifa na Juventus.

Ushindi dhidi ya Juventus uliwapaisha Napoli hadi nafasi ya nne jedwalini kwa alama 40 sawa na AS Roma na Lazio.

Kwa upande wao, Juventus waliokuwa wamepotea alama mbili pekee katika Serie A tangu Disemba 22, kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwa pointi 42, saba nyuma ya AC Milan walioduwazwa kwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa limbukeni Spezia.

MATOKEO YA SERIE A (Februari 13):

Napoli 1-0 Juventus

Spezia 2-0 AC Milan

Torino 0-0 Genoa

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Manchester City wakomoa Spurs na kuendeleza ubabe wao...

JAMVI: Azma ya Mukhisa Kituyi kuwania urais pigo kwa...