• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Bei ya mafuta kupandisha gharama ya maisha

Bei ya mafuta kupandisha gharama ya maisha

Na BENSON MATHEKA

GHARAMA ya maisha nchini inatarajiwa kupanda kwa kiwango kukubwa baada ya Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli (EPRA) kupandisha bei ya mafuta kuanzia jana usiku.

EPRA imeongeza bei ya petroli kwa Sh8.19, dizeli kwa Sh5.51 na mafuta taa kwa Sh5.32 kwa kila lita mwezi mmoja ujao.Ongezeko hilo ndilo la juu zaidi katika kipindi cha miezi sita iliyopita.

Kulingana na Epra, kupanda kwa bei za mafuta kumesababishwa na kuongezeka kwa bei ya bidhaa hiyo ulimwenguni.

Kaimu mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo Daniel Kiptoo, alisema mabadiliko ya thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya dola ya Amerika pia yalichangia ongezeko la bei.

“Katika kipindi hicho kulikuwa na mabadiliko kwa thamani ya sarafu ya Kenya dhidi ya dola ya Amerika,” alisema.

Kuanzia jana usiku, bei ya lita ya petroli aina ya supa iliuzwa kwa Sh112.78, dizeli iliuzwa kwa Sh99.52 nayo lita moja ya mafuta taa iliuzwa kwa Sh90.05 mjini Mombasa. Jijini Nairobi, bei ya lita ya petroli aina ya Supa ni Sh115.18, diseli ni Sh101.91 na mafuta taa yanauzwa kwa Sh92.44 kwa lita.

Katika Kaunti ya Kisumu lita moja ya petroli inauzwa Sh115.76, dizeli Sh102.73 na mafuta taa Sh93.28. Kufuatia ongezeko hilo, gharama ya huduma na bei za bidhaa zinatarajiwa kupanda na kuathiri Wakenya hasa maskini ambao tayari wanakabiliwa na athari za janga la corona.

Watoaji huduma muhimu kama vile umeme na viwanda vinavyounda bidhaa, hupandisha bei kutokana na gharama ya petroli.Isitoshe, Wakenya wengi hutegemea mafuta ya taa na gesi kwa mapishi.

Wahudumu wa magari ya uchukuzi pia hulazimika kupandisha nauli kwa abiria, ili kufidia gharama za utoaji huduma katika sekta hiyo.

You can share this post!

Askofu asema corona imewapa Wakenya fursa ya kumtambua Mola

LEONARD ONYANGO: CBC isiwabague watotowatokao familia...