• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:50 AM
TAHARIRI: Tumbo lisiongoze maamuzi ya BBI

TAHARIRI: Tumbo lisiongoze maamuzi ya BBI

NA MHARIRI

KATIBA ni stakabadhi ambayo hubadilika kulingana na nyakati na mahitaji ya wananchi.

Kinyume na Korani au Biblia ambazo ziliandikwa kuwa ni maneno ya kiroho, Katiba ni kitabu kilichoandikwa na kuacha nafasi ya kubadili mambo kulingana na hali ya kisiasa, kijamii au kiuchumi itakavyokuwa.

Katiba yetu ilipopitishwa mwaka 2010, Sura ya 16 Kifungu cha 255 kilieleza jinsi ambavyo Katiba hiyo inaweza kufanyiwa marekebisho.

Shughuli ya kuirekebisha inaendelezwa kupitia Mswada wa Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2020, maarufu kama BBI. Tayari mabunge matatu ya Kaunti (Kisumu, Siaya na Homa Bay) yamepitisha mswada huo huku Baringo ikiukataa.

Madiwani katika maeneo mbalimbali ya nchi sasa wanasema hawatapitisha mswada huo iwapo hawatapewa pesa. Wale wa magharibi mwa nchi wametangaza hadharani kwamba hawatasikiza wito wowote kutoka kwa upande unaounga mkono mswada huo iwapo hawatapewa pesa.

Wanadai kuwa kwa vile Rais Uhuru Kenyatta na kinara mwenza Raila Odinga waliwaahidi ruzuku ya magari, wanapaswa kutimiza ahadi hiyo kwanza.Hali ni kama hiyo katika kaunti nyingine ambako MCAs wanaonekana kuongozwa na tamaa ya pesa kuliko kuangalia vipengee vya Katiba vinavyolengwa kurekebishwa.

MCAs wanapaswa kujiuliza kama vipengee hivyo vitakuwa na manufaa kwa wananchi au la. Lengo la sheria yoyote ni kurahisisha maisha ya mwananchi.

Wanasiasa katika mabunge ya Kaunti wamejigawa katika vikundi vya wanaounga, wanaopinga na wanaosubiri kupewa pesa. Huu si mwelekeo mzuri kwa viongozi.

Kwanza yafaa wawahusishe wananchi kwa kuwaeleza yaliyomo kisha wawasikize na kuchukua maoni yao. Wakati wa kujadili na kuamua kuhusu mswada huo, viongozi hao wajiulize maswali kadhaa: Je, ni lazima turekebishe katiba sasa? Je, iwapo tutapitisha marekebisho, ni faida zipi au hasara zipi ambazo wananchi watapata?

Kama hawataelewa mswada huo, watafute ufafanuzi kutoka kwa wanasheria wasioegemea upande wowote, ili wafanye uamuzi wakiwa wanajua wanachoamua.

Kupitisha au kukataa mswada huo kwa sababu ya kupewa pesa au kunyimwa hongo ni makosa. Sura ya Sita ya Katiba inasisitiza uadilifu wa viongozi. Mojawapo ya sifa za uadilifu ni kufanya lililo sawa bila ya kushinikizwa na ahadi za pesa au hisia za kibinafsi.

You can share this post!

LEONARD ONYANGO: CBC isiwabague watotowatokao familia...

Hofu wanafunzi hawavai maski wakiwa shuleni