• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:04 PM
BENSON MATHEKA: Wabunge wasitunge sheria kulenga mirengo ya kisiasa

BENSON MATHEKA: Wabunge wasitunge sheria kulenga mirengo ya kisiasa

Na BENSON MATHEKA

WABUNGE watakapojadili mswada unaopendekezwa wa kuharamisha kampeni ya mahasla, wanastahili kufahamu kuwa huenda wakajipata wakijisulubisha wenyewe. Hii ni kwa sababu mswada huo unawalenga wanasiasa kama wao.

Japo inaonekana kama hatua nzuri ya kuzima matamshi ya uchochezi na kusema kweli inafaa, wabunge hawafai kupitisha au kutunga sheria yoyote wakilenga kuzima mrengo fulani wa kisiasa inavyoonekana kwa wakati huu.

Mswada unaopendekezwa na kamati ya usalama wa kitaifa ya bunge unaonekana kulenga kuzima kampeni ya Naibu Rais William Ruto ya kulinganisha watu wa mapato ya chini na matajiri.

Wabunge wanapendekeza mswada ambao utaharamisha kampeni hiyo katika mikutano ya kisiasa.Japo ni hatari kuchochea chuki za matabaka, mswada huo unazima uhuru wa kujieleza na kutoa maoni nchini. Ni kweli uhuru huo unafaa kuwa na mipaka.

Hata hivyo, nchi hii ina sheria nyingi za kukabiliana na wanaokiuka sheria ambazo hazitumiwi kikamilifu. Ni sheria hizi zinazofaa kutumiwa kukabili wanaokiuka sheria badala ya kutunga mpya au kuzibadilisha kulenga mrengo fulani wa kisiasa au makundi ya watu.

Sio mara ya kwanza ambapo wabunge wametumiwa kupitisha sheria ambazo baadaye zinatumiwa kuwahangaisha wanapojiunga na mrengo wa kisiasa ulio na falsafa tofauti na walio mamlakani.

Ni kweli, athari za kampeni ya Dkt Ruto zinaweza kuwa hatari kwa usalama wa nchi kama visa vilivyoshuhudiwa vya uchomaji wa magari ya watu wanaodhaniwa kutoka familia za mabwenyenye waliotumia ushawishi wao kujipatia mali wakiwa mamlakani.

Kuna sheria za kukabiliana na uhalifu wa aina hii kuanzia kwa anayetoa matamshi ya uchochezi na anayetekeleza uhalifu kufuatia matamshi hayo.

Kinachohitajika sio sheria nyingi au kubadilisha sheria zilizoko bali ni kuwa na nia njema ya kutekeleza sheria zilizopo bila ubaguzi. Kubadilisha sheria au kutunga mpya hakuwezi kusaidia iwapo wanaojukumiwa kuzitekeleza hawana nia njema ya kufanya hivyo au wanaagizwa kuzitekeleza kwa ubaguzi kutimiza maslahi ya watu wachache hasa walio mamlakani.

Sio ajabu wabunge watakaounga mswada huo, wakiwemo wanachama wa kamati inayoupendekeza wakajipata wakijilaumu siku zijazo sheria itakayopitishwa ikitumiwa kuwadhulumu.Kamati hiyo inafaa kusisitiza utekelezaji wa sheria zilizopo ikiwemo ya maadili.

Na ikiwa nia ya mswada huo ni kutia nguvu sheria ya Tume ya Uwiano na Utangamano (NCIC), wabunge wasidhani itakuwa ya kukanyagia breki kampeni ya Dkt Ruto pekee., kwa kuwa wao ni wanasiasa kama yeye na wanaweza kujipata katika hali inayomkabili kwa sasa kwa kuwa siasa ni telezi

You can share this post!

Serikali yaonya mvua yaja mwezi ujao kwa kishindo kikuu

Kisiwa cha matajiri ‘kuwafuga’ maskini