• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
COVID-19: WHO yataka mataifa yenye uwezo mkubwa yaache ‘uchoyo’

COVID-19: WHO yataka mataifa yenye uwezo mkubwa yaache ‘uchoyo’

Na MASHIRIKA

BERLIN, Ujerumani

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amesihi mataifa tajiri kujisaili kabla ya kujiagizia chanjo za ziada za Covid-19.

Amezitaka nchi hizo kujiuliza iwapo vitendo vyao vinahujumu juhudi za mataifa fukara kupata chanjo hizo.

Mataifa tajiri yamejitwalia mabilioni ya dozi za chanjo hiyo, baadhi yakiagizia dozi za kutosha kuwachanja raia wake zaidi ya mara moja, huku baadhi ya nchi zinazoendelea zikiwa na dozi chache au hazina kabisa.

Kampeni kabambe ya utowaji chanjo kote duniani inachukuliwa kama hatua muhimu ya kukomesha janga hilo.

Mataifa ya Uropa yametoa msaada wa kifedha kwa mradi wa COVAX unaoungwa mkono na UN, ambao unalenga kutoa chanjo hizo kwa watu wanaozihitaji zaidi ulimwenguni.

Nchi hizo vilevile zinatafakari kugawa baadhi ya chanjo zake binafsi, lakini hazijabainisha wazi ni lini.

Mnamo Ijumaa, Februari 18, viongozi wa Mataifa Kuu 7 yanayotawala viwanda walisema wataharakisha mchakato wa kuunda na kusambaza chanjo duniani na kufadhili “usawa katika usambazaji wa chanjo kwa bei nafuu,” na matibabu ya Covid-19.

G7 ilitaja kukusanya kwa pamoja Sh822.75 bilioni kufadhili juhudi hizo zinazoungwa mkono na UN.

Mkurugenzi wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus, alishukuru G7 kwa nadhiri zao za “kiasi kikubwa.”

“Hata ukiwa na pesa, ikiwa huwezi kutumia pesa hizo kununua chanjo hizo…kuwa na hela hizo hakumaanishi chochote,” alisema Tedros baada ya mazungumzo na Rais wa Ujreumani Frank-Walter Steinmeier, mnamo

Alisema mielekeo ya baadhi ya mataifa tajiri kwa viwanda kwa lengo la kujitwalia chanjo zaidi, “inaathiri maafikiano na COVAX, na hata kiwango kilichotengewa COVAX kilipunguzwa kutokana na vitendo hivyo.”

Alisema kuwa mataifa tajiri yanapaswa “kushirikiana kuhusu kuheshimu maafikiano yaliyofanywa na COVAX” na kuhakikisha kabla ya kuitisha chanjo zaidi, kwamba maombi yao hayahujumu maafikiano hayo.

“Lakini sidhani wanauliza swali hilo,”

“Ikiwa virusi hivi havitashindwa kila mahali, hatuwezi kuvishinda duniani kote. Itakuwa eneo salama mahali fulani lakini vinaweza kuzuka tena,” alisema Tedros.

Alitahadharisha kuwa mataifa yatakayoachwa nyuma katika shughuli ya kutoa chanjo huenda pia yakageuka “vituo vikuu vya aina mpya ya virusi kuzalishana.”

TAFSIRI NA: MARY WANGARI

You can share this post!

BURUDANI: Lonely Man si mpweke

Marcelo Bielsa wa Leeds United kufanya maamuzi kuhusu...