• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 2:25 PM
BURUDANI: Malisaba azidi kukifua kipaji cha uigizaji

BURUDANI: Malisaba azidi kukifua kipaji cha uigizaji

Na JOHN KIMWERE

ANAAMINI anatosha mboga kufanya vizuri katika tasnia ya maigizo na kutinga upeo wa kimataifa miaka ijayo.

Anasema amepania kujituma mithili ya mchwa ili kutimiza ndoto yake katika jukwaa la burudani wala hatokubali chochote kuzima ndoto yake.

Eunice Khasiani Lihanda maarufu Malisaba ni miongoni mwa wasanii wengi tu wanaokuja hapa nchini katika tasnia ya maigizo. Kando na uigizaji dada huyu ni mtunzi wa nyimbo za injili pia anajihusisha na ufungaji wa ng’ombe wa maziwa na kuku wa mayai.

”Ukweli wa mambo sikufahamu kwamba uigizaji utaibuka talanta yangu lakini nakumbuka nilianza kuchekesha wanafunzi wenzangu nilipokuwa nikisoma shule ya msingi,” alisema na kuongeza kuwa baadaye alianza kujituma kwenye jukwaa la uigizaji na uimbaji mwaka 2006.

Eunice Khasiani Lihanda maarufu Malisaba. Picha/ John Kimwere

Anasema alivutiwa na masuala ya uigizaji tangia akiwa mtoto ambapo alipenda sana kutazama mwigizaji mkongwe Mama Kayai aliyekuwa akishiriki kipindi cha ‘Vitimbi’ kilichokuwa kinapeperushwa kupitia runinga ya KBC.

”Siwezi kuweka katika kaburi la sahau kwamba nilikuwa napenda sana kutazama mama Kayai akifanya uhondo wake ambapo nilikuwa nikiambia familia yangu kuwa siku moja nami pia nitashiriki filamu na ifanikiwe kuoneshwa kwenye runinga,” akasema. Msichana huyu anasema serikali imefanya vizuri kuzindua mtaala wa elimu ya CBC ambapo itakuwa rahisi kutambua taaluma za wanafunzi wakiwa wandogo. Kipusa huyu anajivunia kushiriki kipindi cha ‘Vionja mahakamani,’ kati ya 2017 na 2019 kiichokuwa kikipeperushwa kupitia KBC TV.

Pia alibahatika kushiriki filamu kwa jina ‘Mke Sumu’ iliyopata mpenyo kupeperushwa kupitia runinga ya Capuchin TV. Filamu hiyo ilikuwa kati ya kazi za kampuni ya Bahati Zenawood Production. Katika mpango mzima anasema ndani ya miaka mitano ijayo anatamani sana kuwa ameiva kufikia kiwango cha kimataifa.

Eunice Khasiani Lihanda maarufu Malisaba. Picha/ John Kimwere

Katika mpango mzima anasema kuwa amepania kujituma kwa udi na uvumba angalau afikie kiwango cha Mama Kayai. Kisura huyu anasema barani Afrika angependa kufanya kazi na waigizaji wengi tu huku akitaja baadhi yao kama: Wema Sepetu wa Tanzania na Mercy Johnson mwigizaji wa filamu za Kinigeria (Nollywood). Kwa wenzie wa humu nchini angependa sana kushirikiana na Mama Kayai na Brenda Wairimu kati ya wengine.

Anatoa wito kwa kina dada wapendane pia wajitume mithili ya mchwa kama wanaume na wajifunze kuinuana kitalanta na hata kitaaluma nyakati zote.

Changamoto

Anasema kuwa katika sekta ya maigizo wanapitia changamoto nyingi tu ikiwamo kukosa fedha za kugharimia shughuli zao kikazi.

Pia anasema kuwa mwigizaji akipata umaarufu hudhaniwa ana pesa ndefu jambo ambalo sio ukweli siku zote au kila mara. Pia anadokeza kuwa hatua ya wao kuwa mastaa huchangia badhi yao kupandisha kiwango cha maisha yao ilhali hawana kipato cha kugharimia mahitaji yao ipasavyo.

You can share this post!

Kandie, Chelangat waonyesha wenzao kivumbi mbio za mita...

Shujaa na Lionesses wararua wenyeji Uhispania raga ya...