• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 4:43 PM
Kandie, Chelangat waonyesha wenzao kivumbi mbio za mita 10,000 ugani Nyayo

Kandie, Chelangat waonyesha wenzao kivumbi mbio za mita 10,000 ugani Nyayo

Na AYUMBA AYODI

MSHIKILIZI wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21 na mshindi wa medali ya fedha kwenye Riadha za Nusu-Marathon Duniani, Kibiwott Kandie aliibuka mshindi wa mbio za mita 10,000 Jumamosi.

Kwenye duru hiyo ya kwanza ya mbio na fani za uwanjani ya Shirikisho la Riadha Kenya (AK), Sheila Chelangat alitawala mbio za 10,000 za kinadada uwanjani Nyayo.

Kandie mara kwa mara alichukua uongozi wa mbio hizo za mizunguko 25 katika kundi la watu saba lililokuwa mbele.

Kisha, Shadrack Kiphirchir aliongoza kundi la watu watano ikisalia mizunguko sita huku Kandie akishikilia nafasi ya tatu kabla ya kujitosa kileleni ikibaki mizunguko minne.

Vita vya ubingwa vilisalia kuwa kati ya Kandie na Gilbert Kimunyan ikisalia mizunguko miwili. Hata hivyo, Kandie alitumia miguu yake mirefu kufungua mwanya na kukamilisha umbali huo kwa dakika 28:28.0 karibu mita 80 dhidi ya mpinzani huyo.

“Zimekuwa mbio zangu za kwanza uwanjani tangu Julai 2019 na nimeridhika,” alisema Kandie ambaye majuzi aliachilia taji la kitaifa la mbio za nyika alipolemewa na Rogers Kwemoi.

“Nimekuwa nikitatizika tangu mbio hizo za nyika ambazo nilitumia nguvu nyingi, lakini mwili wangu sasa uko sawa,” alisema na kutangaza kuwa vita vyake vya Olimpiki vimeanza rasmi.

Kandie alifichua kuwa sasa nguvu zake zote ataelekeza katika mazoezi makali ya mbio za uwanjani baada ya kutofuata ratiba hiyo kwa muda mrefu.

“Nitazamia sasa mazoezi ya kuzunguka uwanja. Lazima nipate kasi ninayotaka kwenye uwanja,” alisema mtimkaji huyo mwenye umri wa miaka 24 ambaye hajaamua iwapo atashiriki mbio za Istanbul Half Marathon mnamo Aprili 4 ama la.

“Nalenga medali ya dhahabu mjini Tokyo, Mungu akipenda,” alisema Kandie ambaye alimaliza mbele ya Kimunyan kwa sekunde tisa (28:37.7) naye Peter Mwaniki akafunga mduara wa tatu-bora (28:39.7) katika kundi ambalo lilikuwa na wakimbiaji sita waliokuwa na kasi ya juu kabisa.

Emmanuel Kemboi alishinda kundi la pili la mbio za mita 10,000 kwa dakika 29:28.9 na kufuatiwa na Fredrick Mweti (29:40.6).

Malkia wa mbio za nyika nchini Chelangat, ambaye alikuwa amewasili kutoka kambi ya mazoezi ya timu ya Kenya ya mbio za nyika katika Chuo cha Walimu cha Kigari Embu, alitifulia wenzake vumbi akishinda mbio za mita 5,000 kwa dakika 15:42.2.

Jackline Rotich na Mary Nyaruai waliridhika katika nafasi ya pili na tatu kwa dakika 15:49.6 na 15:50.2 mtawalia. “Nitashiriki mashindano mawili ya mbio za nyika nchini Italia mwezi Machi na mbio za leo zimekuwa sehemu ya maandalizi yangu, hasa kwa sababu mbio za nyika za Bara Afrika zinaning’inia,” alisema Chelangat.

Mshikilizi wa rekodi ya kitaifa ya mbio za mita 400 Hellen Syombua pamoja na Evangeline Makena na Gladys Musyoki walishinda makundi yao ya mbio hizo za mzunguko mmoja. Syombua alitumia sekunde 55.17, Makena 55.89 naye Musyoki akaandikisha 55.20.

Joshua Ndombi alitimka sekunde 10.55, akibwaga Hesbon Ochieng (10.57) na kushinda kundi lake la mbio za mita 100 na kufika fainali. Ferdinand Omanyala alishinda kundi la pili kwa sekunde 10.61 naye mkazi wa Amerika Moffat Wanjiru akatikisa katika kundi la tatu (10.75).

You can share this post!

Sagan Tosu anayochezea Mkenya Ismael Dunga yasaga Shonan...

BURUDANI: Malisaba azidi kukifua kipaji cha uigizaji