• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:50 AM
Uhuru huenda apanga kumkweza Gideon kisiasa kurudisha mkono

Uhuru huenda apanga kumkweza Gideon kisiasa kurudisha mkono

Na WANDERI KAMAU

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta kumruhusu Seneta Gideon Moi wa Baringo kusoma taarifa ya pamoja kuwashukuru madiwani kwa kupitisha mswada wa ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI), Alhamisi, imeibua maswali ikiwa kuna mkakati fiche kumkweza kisiasa.

Kikao hicho ambacho kilifanyika katika Ikulu ya Nairobi, kiliwashirikisha vigogo wengine wa kisiasa wakiwemo kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, Bw Kalonzo Musyoka (Wiper), Bw Musalia Mudavadi (ANC), Seneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) na Gavana wa Kitui, Bi Charity Ngilu (Narc).

Ingawa kikao hicho kililenga kuwashukuru madiwani, hatua ya Gideon Moi kusoma taarifa hiyo imezua hisia mseto, baadhi ya wadadisi wakiitaja kama “dalili kuna mpango fiche wa kumkweza Gideon kisiasa.”

Familia za Rais Kenyatta na marehemu Daniel Moi zimekuwa marafiki wa karibu kisiasa, hasa ikizingatiwa Mzee Moi ndiye aliyemleta Rais kwenye ulingo wa siasa mnamo 1999.

Wadadisi wanasema huenda taswira hiyo ikaashiria Rais Kenyatta anapanga “kurudisha mkono” kwa Mzee Moi, kwani mnamo 2002, alimwidhinisha kama mwaniaji urais wa Kanu.

Ni mkakati uliopewa msimbo wa “Project Uhuru” ambao ulikuwa mpango wa kumkweza Uhuru kisiasa na wale waliofasiri hatua ya Mzee Moi kama “kurudisha uongozi” kwa familia ya Mzee Kenyatta.

“Kilicho wazi ni kuwa Rais Kenyatta anafanya kila juhudi kumkweza kisiasa Gideon kama mpango wa kumshukuru babake, Mzee Moi, kwa kumtengenezea njia kisiasa, hadi akafanikiwa kuwa rais,” asema Bw Charles Mulila, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kwa mujibu wa mchanganuzi huyo, ni kinaya kwa Gideon kusoma taarifa hiyo, ikizingatiwa Kaunti ya Baringo ni miongoni mwa zile ambazo ziliiangusha ripoti hiyo, licha ya madiwani kuahidiwa kupewa ruzuku ya Sh2 milioni kununulia magari.

“Rais Kenyatta au Bw Odinga ndio wangeisoma taarifa hiyo, kwani wao ndio wamekuwa katika mstari wa mbele kuipigia debe. Vile vile, ni ripoti inayofasiriwa kuwa ‘mradi’ wao,” akasema Bw Mulila.

Licha ya viongozi katika mrengo wa kisiasa wa ‘Kieleweke’ kupuuzilia mbali madai hayo, wenzao katika kundi la ‘Tangatanga’ wanafasiri hatua hiyo kama njama ya makusudi kumsuta Naibu Rais William Ruto.

Seneta Moi na Dkt Ruto wamekuwa waking’ang’ania ubabe wa kisiasa katika eneo la Bonde la Ufa, ambapo wote wawili wametangaza azma ya kuwania urais mwaka ujao.

“Taswira hiyo ilimlenga Dkt Ruto kuwa kwanza, yeye si sehemu ya mpango huo. Pili, bado kuna nafasi ya kumtengenezea njia Gideon hata ikiwa atakataliwa kwao,” asema Bw Dismus Mokua, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Licha ya hayo, Dkt Ruto amesema hajali mikakati inayopangwa na washindani wake, akisisitiza kuwa hatalegeza azma yake kuwania urais kwenye uchaguzi.

Waandani wake pia wamesema hawatatikiswa kisiasa na mikakati yoyote ikayayoendeshwa kuwalenga.

“Kufikia sasa, hakuna lolote linalotutia hofu. Tumeona mengi japo tuko tayari kuyakabili,” akasema mbunge Rigathi Gachagua (Mathira), ambaye ni miongoni mwa washirika wa karibu wa Dkt Ruto.

You can share this post!

Wakazi sasa kusafisha jiji kila mwezi

Amevutia Wakenya kwa kuongea Kiswahili sanifu