• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Bale angali tegemeo kubwa kambini mwa Spurs – Mourinho

Bale angali tegemeo kubwa kambini mwa Spurs – Mourinho

Na MASHIRIKA

MKUFUNZI Jose Mourinho amesema fowadi Gareth Bale ana uwezo wa kutamba katika kikosi chochote duniani kwa sasa na Tottenham Hotspur wanahitaji sana maarifa yake katika kila mchuano wa msimu huu.

Hii ni baada ya sogora huyo raia wa Wales kufunga mabao mawili mnamo Februari 28, 2021 na kusaidia waajiri wake Spurs kuponda Burnley 4-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Magoli mengine ya Spurs katika mchuano huo yalifumwa wavuni kupitia nahodha Harry Kane na kiungo Lucas Moura.

Baada ya kushindia Real Madrid mataji manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), mengi yalitarajiwa sana kutoka kwa Bale aliyerejea kambini mwa Spurs mwanzoni mwa msimu huu baada ya kuagana na Real kwa mkopo.

Akiwa Spurs, Bale alitawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka mara mbili kabla ya kutua Uhispania kuvalia jezi za Real.

Hata hivyo, baadhi ya kampeni zake katika La Liga zilivurugwa na visa vya majeraha, jambo lililomchochea kocha Zinedine Zidane wa Real kumtema katika kikosi chake.

Lakini Bale kwa sasa ameokena kufufua makali yake na alifunga mabao mawili dhidi ya Burnley siku saba baada ya kufunga mara mbili (nyumbani na ugenini) na kuongoza Spurs kuwabandua Wolfsberger ya Austria kwenye Europa League kwa mabao 8-1.

Mechi dhidi ya Burnley mnamo Februari 28 ilikuwa yake ya tatu akipangwa katika kikosi cha kwanza cha Spurs ligini msimu huu. Bale, 31, alihitaji sekunde 70 pekee za mwanzo wa kipindi cha kwanza kucheka na nyavu za wageni wao.

Spurs walijibwaga ugani wakijivunia motisha ya kushinda Burnley 5-0 katika mchuano mwingine uliowakutanisha na kikosi hicho cha kocha Sean Dyche katika kampeni za msimu wa 2019-20 nyumani kwao.

Spurs walishuka dimbani kwa ajili ya gozi dhidi ya Burnley wakiwa rekodi mbovu ya kupoteza mechi tano kati ya sita za awali.

Ushindi waliousajili uliwapaisha hadi nafasi ya nane jedwalini kwa alama 39 sawa na Aston Villa. Ni pengo la alama sita ambalo kwa sasa linawatenganisha Spurs na nambari nne West Ham United.

Tangu arejee kambini mwa Spurs mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20, Bale alikuwa amewajibishwa katika mechi mbili za EPL na mabao matatu kati ya manne aliyofungia waajiri wake yalitokana na mechi za kuwania makombe tofauti, si EPL.

Mnamo Februari 17, 2021, Bale alisema kwamba hakuwa akicheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza cha Spurs kwa sababu alikuwa “akikaribia mwisho wa kutamba kwake kwenye ulingo wa usogora.”

Hata hivyo, siku 11 baada ya kutoa kauli hiyo, mwanasoka huyo amecheza mechi nne, kupachika wavuni mabao manne na kuchangia mengine matatu kambini mwa Spurs.

Katika kipindi cha miaka saba akivalia jezi za Real, Bale alifunga jumla ya mabao 105 na kuongoza mabingwa hao watetezi wa La Liga kutwaa mataji manne ya UEFA.

Ufufuo wa makali ya Bale ni jambo ambalo kwa sasa linatarajiwa kutiwa mizani na mashabiki katika mechi mbili zijazo dhidi ya Fulham na Crystal Palace mnamo Machi 3 na 7 mtawalia.

Kwa upande wao, Burnley wataalika Leicester City uwanjani Turf Moor mnamo Machi 3 kabla ya kuvaana na Arsenal siku tatu baadaye. Kikosi hicho kwa sasa kinashikilia nafasi ya 15 jedwalini kwa alama 28 baada ya mechi 26.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Washtakiwa kulangua raia wa Burundi

Raia wa Sudan ndani kwa kukaidi kulipa deni