• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Kingi amzima Raila

Kingi amzima Raila

CHARLES LWANGA na WINNIE ATIENO

GAVANA wa Kilifi, Bw Amason Kingi jana alimfokea hadharani kinara wa ODM, Bw Raila Odinga kwa kupinga mpango wa wakazi wa Pwani kuunda chama chao cha kisiasa.

Bw Kingi aliye gavana aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha ODM, alisema ni kejeli kwa Bw Odinga kuwakataza Wapwani kuwa na chama chao, ilhali vyama kama Amani National Congress (ANC), Wiper, Ford-K na United Demoratic Alliance (UDA), vinajulikana ni vya maeneo gani.

Alishangaa ni kwa nini Wapwani wakiungana pamoja kupitia nyama vidogo kama vile Kadu Asili, Shirikisho, Devolution na Umoja Summit, inadaiwa kuwa hatari kwa usalama ilhali maeneo mengine ya Kenya yameunda vyama vya kimaeneo.

“Mbona Pwani ikiungana ili kujipanga kisiasa kupitia kwa mrengo, inasemekana ni hatari na yenye nia ya kuleta uhasama baina ya wakazi na kutenganisha Wakenya? Huko magharibi kuna Musalia Mudavadi na Moses Wetangula ambao wameungana japo wako kwa vyama tofauti, lakini wameungana kisiasa kuwakilisha watu wao,” akasema.

Hapo awali katika mkutano eneo la Ganze, Bw Odinga alikuwa amekashifu wito wa kuunda chama cha pwani akisema kuwa hatua hiyo ni yenye nia ya kuwatenganisha wananchi kimaeneo na badala yake akawasihi wakazi waungane pamoja naye katika chama ODM.

“Bw Kingi ni rafiki yangu niliyemkaribisha katika siasa mwaka wa 2007, ambapo nilimpa nafasi ya uwaziri hadi mwaka wa 2013 ugatuzi ulipokuja nilipomwambia akatumikie watu wake na kumpa usaidizi wangu katika ODM,” alisema.

Bw Odinga aliuliza ni upi ubaya wa ODM ambao umemfanya Bw Kingi kutaka kuhama chama hicho na kuunda chama au mrengo wa Wapwani ili kukitumia kwa uchaguzi ujao. Alishangaa kwa nini hivyo ilhali amekuwa akichaguliwa kupitia ODM tangu mwaka wa 2007 hadi 2017.

“ODM ilikuwa mbaya lini ambapo anataka kuhama?” alisaili na kuongeza, “Si vyama vya Shirikisho na Kadu-Asili vimekuwapo tangu miaka hiyo yote akielekea uchaguzi ambapo amekuwa akigombea kwa ODM? Tangu lini ODM imekuwa mbaya? Mbona hakugombea kwa hivyo vyama vingine?”

Vilevile Bw Odinga aliwataka wanasiasa wakumbatie umoja badala ya kutenganisha wananchi katika siasa za vyama.

“Vyama vya kiasasa havifai kufungiwa katika ngome fulani. Bw Joho ambaye ni naibu wa ODM anatoka Mombasa na mwenzake, Gavana wa Kakamega Wyclife Oparanya anatoka Kakamega. Hii ndiyo sura ya chama cha kitaifa. Tuache kufananisha viongozi wa vyama vya kitaifa na ngome zao. Leo hii Bw Kingi akiwa kinara wa ODM, hatuwezi kusema ngome ya ODM ni Kilifi.”

Mbunge wa Ganze, Bw Teddy Mwambire alikuwa amemhakikishia Bw Odinga kuwa licha ya siasa za vyama, wakazi wa Pwani hawamtoroki lakini wanapiga hesabu za kuhakikisha wamewakilishwa katika jukwaa la siasa za kitaifa.

Mbunge wa Rabai, Bw William Kamoti naye alisema baadhi ya maeneo mengine nchini yamewakilishwa na vinara wawili wala hakuna kosa kwa eneo la Pwani kuungana na kuwakilishwa katika siasa za kitaifa.

“Hivi majuzi baada ya mkutano wa ikulu jijini Nairobi ulioitishwa na Rais Uhuru Kenyatta, taswira iliyotokea ilionyesha kuwa maeneo mengine yana vinara wawili, ambalo si kosa. Mbona sasa imekuwa mjadala baada ya Pwani kuungana?” akauliza.

You can share this post!

Mwalimu amkata mwenzake wakipigania msichana wa chuo

Kibo Queens invyokuza vipaji kuwa mastaa