• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Chelsea wakomoa Everton na kuweka hai matumaini ya kumaliza msimu huu wa EPL ndani ya 4-bora

Chelsea wakomoa Everton na kuweka hai matumaini ya kumaliza msimu huu wa EPL ndani ya 4-bora

Na MASHIRIKA

CHELSEA walifunga bao katika kila kipindi na kupepeta Everton ambao ni washindani wao wakuu katika vita vya kupigania nafasi ya kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ndani ya mduara wa nne-bora muhula huu.

Chini ya kocha Thomas Tuchel, Chelsea waliokuwa wenyeji wa mechi hiyo waliwekwa na beki Ben Godfrey wa Everton aliyejifunga baada ya mpira uliopigwa na kiungo Kai Havertz kumzidi ujanja katika dakika ya 31.

Bao la pili la Chelsea lilifumwa wavuni kupitia penalti ya Jorginho Luiz Frello katika dakika ya 65. Mkwaju huo ulichangiwa na tukio la kipa Jordan Pickford kumchezea Havertz visivyo ndani ya kijisanduku cha Everton.

Mchuano huo uliendeleza rekodi nzuri ya Tuchel ambaye kwa sasa amesimamia jumla ya mechi 11 za Chelsea bila ya kupoteza yoyote tangu aaminiwe fursa ya kuwa mrithi wa mkufunzi Frank Lampard mnamo Januari 2021.

Chelsea wangalifunga mabao mabao zaidi katika kipindi cha kwanza ila makombora yao yakadhibitiwa vilivyo na Pickford. Kati ya masogora wa Chelsea waliomshughulisha zaidi kipa huyo raia wa Uingereza ni Marcos Alonso, Havertz, Callum Hudson-Odoi, Timo Werner na Christian Pulisic.

Zikisalia mechi 10 pekee kwa kampeni za EPL msimu huu kutamatika rasmi, Chelsea kwa sasa wanashikilia nafasi ya nne jedwalini kwa alama 50 na wako pazuri zaidi kuwa miongoni mwa vikosi vitakavyofuzu moja kwa moja kunogesha kampeni za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Ni pengo la alama nne pekee ndilo linatanganisha Chelsea na nambari mbili Manchester United ya kocha Ole Gunnar Solskjaer. Leicester City ya mkufunzi Brendan Rodgers inashikilia nafasi ya tatu kwa pointi 53 huku pengo la alama 12 likitamalaki kati yao na viongozi wa jedwali Manchester City.

Chini ya kocha Carlo Ancelotti, Everton wanakamata nafasi ya sita kwa alama 46, mbili nyuma ya nambari tano West Ham United waliowakung’uta Leeds United 2-0 katika mechi nyingine ya EPL mnamo Jumatatu usiku.

Aston Villa, Tottenham Hotspur na mabingwa watetezi Liverpool ndivyo vikosi vingine vinavyopigania nafasi ya kufuzu kushiriki soka ya bara Ulaya muhula ujao.

Chelsea kwa sasa hawajashindwa katika mechi yoyote tangu wapokezwe kichapo cha 2-0 kutoka kwa Leicester mnamo Januari 19, 2021 chini ya Lampard aliyekuwa mchezaji wao wa zamani.

Chelsea wamenogesha kivumbi cha UEFA mara 15 kutokana na misimu 17 iliyopita na walikuwa wakishikilia nafasi ya tisa kwenye jedwali la EPL huku pengo la alama nne likitamalaki kati yao na West Ham waliokuwa katika nafasi ya nne wakati walipomfurusha Lampard mnamo Januari.

Mabingwa hao wa zamani wa EPL sasa wanajivunia ufufuo mkubwa chini ya Tuchel na ufanisi dhidi ya Everton unamaanisha kwamba sasa wameshinda mechi sita na kusajili sare mara tatu kutokana na mechi tisa ambazo Tuchel amezisimamia ligini kufikia sasa.

Mechi mbili nyinginezo ambazo Tuchel ameongoza Chelsea kushinda ni katika kampeni za Kombe la FA na UEFA.

Mkufunzi huyo raia wa Ujerumani aliwaongoza Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa kutinga fainali ya UEFA mnamo 2019-20 ila masogora wake wakazidiwa maarifa na Bayern Munich. Alikifanyia kikosi alichokitegemea dhidi ya Everton mabadiliko matano kutoka kile kilichocharaza Liverpool 1-0 katika mechi ya awali iliyochezewa ugani Anfield mnamo Machi 4, 2021.

Chelsea kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Leeds United uwanjani Elland Road mnamo Machi 13 kabla ya kualika Atletico Madrid kwa minajili ya marudiano ya hatua ya 16-bora kwenye gozi la UEFA mnamo Machi 17.

Baada ya hapo, wameratibiwa kuchuana na Sheffield United katika robo-fainali za Kombe la FA mnamo Machi 21.

Kwa upande wao, Everton watakutana na Burnley ligini mnamo Machi 13 kabla ya kuwaalika Man-City kwenye robo-fainali ya Kombe la FA mnamo Machi 20 ugani Goodison Park, Uingereza.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Shujaa, Lionesses waanza kujinoa tena baada ya kupumzika...

Mtihani wa gredi ya nne wakumbwa na matatizo maeneo mengi...