Seneta ashtakiwa kwa wizi wa mabavu

Na SHABAN MAKOKHA

SENETA Cleophas Malala wa Kakamega, Jumatano aliachiliwa na mahakama kwa dhamana ya Sh2.5 milioni kuhusiana na ghasia zilizotokea kwenye uchaguzi mdogo wa Matungu wiki iliyopita.

Bw Malala alifikishwa mahakamani pamoja na watu wengine saba na kufunguliwa mashtaka tisa, yakiwemo wizi, kuwashambulia wapinzani wake na matumizi ya nguvu wakati wa uchaguzi huo.

Bw Malala alikabiliwa na mashtaka manne ya wizi wa kutumia mabavu, uharibifu wa mali na kuwashambulia watu akishirikiana na wengine.

Mahakama iliambiwa kuwa washtakiwa walimpora Bw Nabii Nabwera Sh100,000 na Bw Cleophas Shimanyula Sh200,000 katika kijiji cha Mira, eneo la Matungu.

Mnamo Jumatatu, Bw Malala alijisalimisha kwa polisi mjini Kakamega, ambapo alihojiwa kwa karibu saa tatu kabla ya kuachiliwa kwa dhamana ya polisi.

Mlinzi wake, Joel Wekesa, pia alifunguliwa mashtaka mawili tofauti. Alikabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya bunduki na kumshambulia Bw Boniface Oduor katika kituo cha kupigia kura cha Munami.

Wengine walioshambuliwa pamoja naye ni Ababu Shago, Cecil Ambeyi, Shakila Amboye, Marvin Kombo, Joyce Khavere na Kim Ambani.

Kwenye shtaka la kwanza, Bw Malala pamoja na Mabwana Wekesa, Shago, Ambeyi, Kombo, Amboye, Khavera na Ambani walikabiliwa na tuhuma za wizi wa chombo cha kuwekea simu moto chenye gharama ya Sh8,000.

Vile vile, walikabiliwa na mashtaka ya kupanga njama ya kuvuruga amani wakati wa uchaguzi huo, kumshambulia Bi Maurine Naliaka (aliyekuwa akisimamia uchaguzi katika kituo cha kupigia kura cha Munani), kumjeruhi na kutumia nguvu dhidi yake ili kumshurutisha kumpendelea mwaniaji ubunge wa chama cha Amani National Congress (ANC).

Wakiwa mbele ya Hakimu Mkuu Dofina Alago, washtakiwa walikana mashtaka hayo yote na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 kila mmoja na mdhamini wa kiasi kama hicho. Kesi hiyo imepangiwa kutajwa mnamo Machi 25 na kusikilizwa mnamo Juni 22 mwaka huu.