• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 5:26 PM
Msaidizi wa mbunge wa Maragua adai alishambulia mfanyakazi wa Kenya Power kwa ‘nia njema kulinda maslahi ya kijamii’

Msaidizi wa mbunge wa Maragua adai alishambulia mfanyakazi wa Kenya Power kwa ‘nia njema kulinda maslahi ya kijamii’

Na MWANGI MUIRURI

POLISI katika Kaunti ndogo ya Murang’a Kusini wanafanya uchunguzi kumhusu msaidizi wa mbunge wa Maragua aliyenaswa katika picha ya video akimshambulia mfanyakazi wa kampuni ya umeme nchini – Kenya Power – na hatimaye kudai alifanya hivyo kwa nia njema ili kulinda maslahi ya umma.

Bw Martin Wamwea Mburu akiwa msaidizi katika timu ya mbunge Bi Mary Wa Maua ya kampeni alisema kuwa mfanyakazi huyo wa KP alishindwa kujitetea au kujitambulisha “na ndipo nikiwa na uwajibikiaji wa kulinda masilahi ya umma mashinani, nikamsakama.”

Katika ukanda huo Bw Wamwea anaonekana akiwa amembwaga chini mfanyakazi huyo wa kiume wa KP huku akiwa amemthibiti vilivyo katika kichaka, kukiwa na mashahidi kadhaa, kwa upande mwingine wanawake wawili, mmoja akiwa ni mamake mzazi, wakionekana kumsihi aache kushambulia mwanamume huyo aliye hoi.

“Wamwea acha…utajiletea maneno mengi kwa kitendo hiki…acha tu tungoje wakubwa wake waje tuongee,” mama mmoja anasikika akimsihi.

Katika ukanda huo pia kuna mwanamke anayesikika akipiga simu akiomba usaidizi wa dharura uletwe “kwa kuwa mfanyakazi wetu anapigwa na mteja.”

Hapo Jumatano, Bw Wamwea aliambia Taifa Leo kuwa alitekeleza adhabu hiyo kwa kuwa “katika kijiji chetu kumekuwa na visa vya wakora kujifanya wafanyakazi wa shirika la Kenya Power na kutapeli wanavijiji.”

Alisema kuwa alipigiwa simu akaambiwa kuwa “katika boma langu binafsi kulikuwa na mtu aliyekuwa akidai ni mfanyakazi wa KP na ambaye tayari alikuwa amekatiza huduma za umeme akidai kuwa nilikuwa nimeziunganisha kwa njia ya ukora.”

Alisema kuwa alikimbia nyumbani na kupata mwanamume huyo ambaye baada ya kuambiwa ajitambulishe alionekana kutaka kusepa “na sikuwa na budi ila tu kumsakama na kumthibiti nikingoja wakubwa wake au maafisa wa polisi watokee ili kuweka hali wazi na ukweli ubainike.”

Hata hivyo, maafisa wa kiusalama wa KP ndio walifika kwanza na wakamthibiti Bw Wamwea na ambapo aliwekwa pingu na kusafirishwa hadi katika kituo cha doria za polisi cha Kagaa na akafungiwa hapo.

Muda mfupi baadaye Mbunge wa Maragua Bi Wa Maua alifika na kukazuka patashika ya maneno huku maafisa wa polisi wakisisitiza kuwa Bw Wamwea alikuwa mshukiwa wa fujo dhidi ya mlalamishi ambaye kwa sasa alikuwa ashatambulika kama Bw David Muiruri.

Bi Wa Maua alisikika katika nakala ya kurekodiwa kuhusu maongezi akisema kwamba “unajua mimi hufanya kazi katika bunge ambapo sheria hutungwa na la mno, niko katika kamati ya bunge kuhusu kawi na ina maana sheria hizi zote ninazielewa.”

Bi Wa Maua anasikika akisema kuwa katika hali hiyo, “ni aidha mtuandikie bodi ili Bw Wamwea aachiliwe ndio tukafanye kesi katika kituo halisi cha polisi au kortini na mambo hayo mengine yafuate…hapa ni Kenya.”

Maafisa wa polisi wanasikika wakishikilia kuwa hawakuwa na uwezo wa kutafsiri sheria au kupendekeza ni nani alikuwa amekosa “kwa kuwa kuna mikakati ya kufuatwa…hapa hatufanyi kesi za sekta ya kawi bali tunakabiliwa na malalamishi ya mtu kushambuliwa na ambapo ataandaliwa stakabadhi za kimatibabu na hatimaye kesi ifanyike.”

Hatimaye, Bw Wamwea alipewa bodi ya Sh10,000 huku Bw Muiruri akitarajiwa kwenda hospitalini kukaguliwa na kutibiwa majeraha yake na hatimaye akiamua kuendelea mbele na kesi, Bw Wamwea akamatwe upya na afikishwe mahakamani.

Alhamisi, Mkuu wa Kiusalama eneo la Kati Bw Wilfred Nyagwanga alisema ako na ufahamu wa kesi hiyo na anafuatilia.

“Ndio, niko na ufahamu wa kisa hicho, ninajua mshukiwa ameachiliwa kwa bodi ya Sh10,000 na mlalamishi anakimbizana na ukaguzi na tiba hospitalini. Mlalamishi akiamua kuendelea mbele na kesi, ataendelea na tutamkamata mshukiwa na tumuasilishe mahakamani,” akasema.

Mnamo Oktoba 22 mwaka jana, Bi Wa Maua alivamia kituo cha polisi cha Maragua baada ya msaidizi wake mwingine Bw Derick Kibe kukamatwa.

Bw Kibe alikuwa amekamatwa kwa madai ya kueneza uvumi katika mtandao wake wa kijamii ambapo alidaiwa kutoa habari za uongo kuhusu maafisa wa polisi wa Maragua.

Bi Wa Maua alifika katika kituo hicho akiwa mwingi wa hamaki na ambapo alimsakama kamanda Francisca Mbinda akimdai kuendeleza hujuma za kisiasa dhidi yake.

Aidha, alidai kuwa maafisa hao walikuwa wamechukua Sh5,000 kutoka kwa Bw Kibe kwa nia ya kuzifisadi.

Hapo jana, mwenyekiti wa wawakilishi wa Wadi wa Mlima Kenya Bw Charles Mwangi na aliye pia mwakilishi wa wa wadi ya Ichagaki katika eneobunge la Maragua alikashifu “tabia na mienemdo ya Bi Wa Maua.”

Bw Mwangi alisema “hatutakubali maafisa wa usalama katika eneo hili wawe wakiishi kwa hofu ya kulinda sheria isivunjwe hata ikiwa washukiwa ni wafanyakazi wa afisi za kisiasa.”

Bw Mwangi alisema haki inafaa kusawazisha watu wote “na ni makosa makuu kwa yeyote kuzindua njama za kujiangazia kama aliye juu ya sheria.”

  • Tags

You can share this post!

FAIDA YA UBUNIFU: Hajuti kuacha kazi ya benki na kujiajiri...

Seneta ashtakiwa kwa wizi wa mabavu