• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Ulipata alama ya D KCSE? Huenda usiruhusiwe kujiunga na polisi

Ulipata alama ya D KCSE? Huenda usiruhusiwe kujiunga na polisi

Na MARY WANGARI

WANAFUNZI wanaopata alama ya D hivi karibuni hawataweza kujiunga na kikosi cha polisi nchini ikiwa mikakati ya Waziri wa Usalama wa Nchi, Fred Matiang’i itatekelezwa.

Akizungumza mnamo Ijumaa, Machi 12, 2021, jijini Nairobi, Waziri Matiang’i alisaili kuhusu masharti yanayowataka makurutu wanaotaka kujiunga na kikosi cha polisi kuwa na alama kuanzia D katika Cheti cha Mtihani wa Elimu ya Sekondari (KCSE).

Huku akitangaza mipango ya serikali ya kufanyia mageuzi Huduma ya Polisi Nchini (NPS), alisisitiza kuwa kiwango duni cha elimu miongoni mwa walinda usalama kinalemaza uwezo wa polisi kukabiliana na masuala tata ya kiuhalifu.

“Acha niseme wazi na siwazomei maafisa wenzangu wa polisi. Raslimali tunazohitaji hazipo kwa sababu hatuwezi kutumai kuwa makonstebo tuliowapa mafunzo Kiganjo ndio watakaoshughulikia masuala tata tunayojadili ili kusaidia DPP na kesi ya ubakaji,”

“Kusema kweli, kama tunakuajiri ukiwa na alama ya D plus kisha tunakuagiza shughulikie sayansi tata ya kutathmini damu na uandae ripoti itakayotumiwa na DPP kortini kuthibitisha mauaji, tunamaanisha kweli, huo si mchezo?” alisaili Dkt Matiang’i.

Waziri alikuwa akizungumza katika hafla ya kufuzu iliyoandaliwa katika Taasisi ya Mafunzo kuhusu Uendeshaji Mashtaka, eneo la Loresho, Nairobi.

Alieleza kuna mikakati ya kuwajumuisha wataalam katika NPS kama vile madaktari na mawakili katika juhudi za kukabiliana na wahalifu nchini.

“Tumeanza mageuzi mapya katika idara ya polisi. Kwa mara ya kwanza tumeanza kuteua mahafala watakaopatiwa mafunzo kama kama maafisa wa polisi. Watakaokuja kutoka taaluma nyinginezo ni sharti wawe wamesajiliwa katika taaluma zao.

“Mawakili tutakaowaajiri ni sharti wawe tayari wanachama wa Shirika la Mawakili Nchini LSK, na mawakili wa Mahakama Kuu ya Kenya na madaktari tutakaoajiri ni sharti wawe wamefuzu katika taaluma zao. Ili tuanze kutoa mafunzo kwa timu thabiti ya wataalam itakayotimiza kiwango cha Mfumo wa Haki dhidi ya Uhalufu,” alifafanua.

Matiang’i aliyewahi kuhudumu kama waziri wa elimu, alisisitiza umuhimu wa kuinua viwango vya elimu vinavyohitajika kabla ya kuajiri maafisa wa elimu.

“Ndiposa nimekuwa nikipigania kwamba tutazame alama inayohitajika kabla ya kuteua makurutu. Wakati umewadia tukabili uhalisia na kufahamu kuna changamoto ambazo ni sharti tuzikabili kwa kumaanisha,”

“Sisemi kwamba watu wengine hawana maana lakini kuna mambo mengi ya kufanya. Tunahitaji nguvu mpya katika utekelezaji sheria ili unapopatiwa faili hutasema hatuna ujuzi,” alisistiza

You can share this post!

Man-United kumtia mnadani kipa David de Gea mwishoni mwa...

Rais akiri wanasiasa waeneza Covid