• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 5:03 AM
Man-United kumtia mnadani kipa David de Gea mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21

Man-United kumtia mnadani kipa David de Gea mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United watakuwa radhi kupokea ofa kutoka kwa vikosi vitakavyokuwa radhi kumsajili kipa David de Gea mwishoni mwa msimu huu.

Japo De Gea kwa sasa ndiye kipa chaguo la kwanza kambini mwa Man-United, kocha Ole Gunnar Solskjaer amefichua mipango ya kumkweza chipukizi Dean Henderson kuwa mlinda-lango wao nambari moja ugani Old Trafford kuanzia muhula ujao.

Henderson amekuwa akisajili matokeo ya kuridhisha sana katika mechi anayochezeshwa na Man-United tangu kipindi chake cha mkopo kikamilike kambini mwa Sheffield United.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, hali hiyo inasaza De Gea ambaye ni raia wa Uhispania katika ulazima wa kuondoka na tayari ameanza kuhusishwa pakubwa na uwezakano wa kuyoyomea Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa iwapo kocha Mauricio Pochettino hatafaulu kumsajili Hugo Lloris wa Tottenham.

Ingawa kipa Keylor Navas wa PSG anazidi kudhihirisha umahiri wake katikati ya lango la PSG, Pochettino amesema angetamani kujivunia huduma za makipa mawili wa haiba kubwa ili kuweka hai matumaini ya kikosi chake kujizolea takriban kila taji la kivumbi wanachokinogesha.

Maamuzi ya Solskjaer kumtia De Gea mnadani ni zao la presha kutoka kwa Henderson, 23, ambaye ametishia kuondoka na kutafuta hifadhi kwingineko iwapo hatahakikishiwa nafasi ya kuunga kikosi cha kwanza msimu ujao wa 2021-22.

Msimamo wa Henderson unawiana na ule uliochukuliwa na aliyekuwa kipa wa Arsenal, Emiliano Martinez mwishoni mwa msimu wa 2019-20 kabla ya kuachiliwa kujiunga na Aston Villa. Martinez alidai kufanywa kipa chaguo la kwanza mnamo 2020-21 badala ya Bernd Leno wa Ujerumani.

Tottenham pia wanahemea maarifa ya Henderson ili awe kizibo cha Lloris iwapo kipa huyo raia wa Ufaransa atahiari kuungana na Pochettino kambini mwa PSG.

De Gea amekuwa kambini mwa Man-United kwa takriban miaka 10 sasa na kushuka kwa ubora wa fomu yake ni suala ambalo linasaza mustakabali wake kitaaluma katika shaka.

Kubwa zaidi ambalo huenda likachochea Man-United kumwachilia De Gea ni ukubwa wa gharama wa kumdumisha kifedha ikizingatiwa kwamba kipa huyo wa zamani wa Atletico Madrid kwa sasa analipwa mshahara wa Sh52.5 milioni kwa wiki ugani Old Trafford.

De Gea amechezea Man-United katika jumla ya mechi 434 na matokeo yake yalimfanya kuwa miongoni mwa makipa bora zaidi duniani.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Eric Omondi anyenyekea, aahidi kuondoa mtandaoni video chafu

Ulipata alama ya D KCSE? Huenda usiruhusiwe kujiunga na...