• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:55 PM
Walimu wote wepewe chanjo ya Covid-19 bila ubaguzi

Walimu wote wepewe chanjo ya Covid-19 bila ubaguzi

Na WANTO WARUI

HUKU sekta ya elimu ikiwa katika mstari wa mbele kufaidika kwa chanjo ya Covid-19, kuna uwezekano kuwa chanjo hiyo haitawafikia walimu wote nchini hasa wale wanaotoka sekta ya kibinafsi.

Kutokana na idadi kubwa ya walimu nchini ya takriban 350,000 huenda baadhi ya walimu wakatengwa na kukosa kupata chanjo hiyo muhimu. Walimu hutangamana zaidi na watu wengi mitaani licha ya kuwa na wanafunzi shuleni ambao huwa wametoka katika familia tofauti.

Mwalimu anapokuwa darasani yuko katika hatari kubwa sana ya kuambukizwa au kuambukiza maana anatangamana na wanafunzi wengi ambao wametoka nyumbani.Haya yanajiri wakati ambapo walimu wanawaanda wanafunzi ili wafanye mitihani yao ya kitaifa ya darasa la nane, KCPE na kidato cha nne, KCSE.

Kipindi hiki ambapo walimu huenda kupokezwa mitihani hiyo kutoka vituo mbalimbali kote nchini huwa wanakutana katika mikusanyiko mikubwa ambayo ni hatari katika kusambaza ugonjwa wa Covid-19.Tayari kuna idadi kubwa ya walimu ipatayo 25,000 ambao wana umri wa miaka 58.

Kando na hawa, kuna wengine ambao wanaugua maradhi mengine kama vile kisukari na shinikizo la damu. Hawa wote wanahitaji kushughulikiwa kwa dharura.

Sekta ya elimu tayari imekumbwa na misukosuko ya Covid-19 na walimu kadhaa wamefariki.Ijumaa iliyopita, chanjo dhidi ya Covid-19 ilianza kupewa walimu katika makao makuu ya Tume ya Huduma kwa walimu nchini, TSC, jijini Nairobi. Bi Nancy Macharia na wakuu wengine wa idara mbalimbali katika sekta ya elimu walihudhuria kuanzishwa kwa shughuli hiyo.

Chanjo hiyo inafaa iwafikie walimu wote kote nchini bila ubaguzi ikiwemo wale wa shule za kibinafsi na wa shule za Chekechea.

Itakumbukwa kuwa wakati ugonjwa wa Covid-19 ulipoingia nchini, shule zote zilifungwa ghafla. Serikali iliendelea na mpango wake wa kuwalipa walimu wa shule za umma mishahara huku wale wa shule za kibinafsi wakitaabika kwa kukosa lishe, malipo ya kodi na mahitaji mengine ya kimsingi.

Jambo ambalo liliudhi ni kuwa walimu wao hao walioachwa kutaabika hulipa ushuru kwa serikali na kusaidia sana katika kuendeleza elimu nchini.Hii ndiyo maana ni muhimu sana inapofikia suala kama hili la usalama wa wananchi, serikali inatarajiwa kuwahudumia wote katika sekta husika bila ubaguzi.

Ikiwa chanjo hiyo haitatosha walimu wote, kunahitajika kuwe na mpango maalumu wa kuwapa walimu chanjo kwa awamu mbili au tatu. Ni katika uwajibikaji kama huu tu ambapo wananchi huhisi kuwa wote ni raia wa taifa moja. Hili huleta utangamano na umoja nchini la sivyo wananchi wengine hujihisi kama wamesalitiwa katika taifa lao.

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Rais Kenyatta, Mama wa Taifa na Kagwe sasa...

Binti wa chuo aeleza anavyovuna Sh300,000 kila mwezi...