• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Binti wa chuo aeleza anavyovuna Sh300,000 kila mwezi kutokana na useremala

Binti wa chuo aeleza anavyovuna Sh300,000 kila mwezi kutokana na useremala

Na MAGDALENE WANJA

Alipokuwa mchanga, Bi Parky Kamau alikuwa na mazoea ya kuandamana na mamaye kuelekea sokoni Gikomba ambako alipenda kununua nguo za mitumba za kuuza.

Hii ndio biashara ambayo mamake alifanya kwa muda mrefu ili kukimu mahitaji ya jamii yake. Bi Kamau aliandamana naye wakati wa likizo za shule na aliweza kujifunza mengi kuhusu biashara.

Hata hivyo, kuna kitu kilimvutia sana katika soko hilo. Samani za kupendeza zilizotengenezwa na kuuzwa katika soko la Gikomba ambazo mzazi wake hangemudu kuzinunua wakati ule.

“Nilizitamani fanicha hizo sana kama vile viti vilivyokuwa vimeundwa kwa vitambaa vyenye rangi mbali mbali. Wakati mwingine nilienda kutazama mafundi hao wakitengeneza na nikatamani sana kufanya biashara hio, alisema Bi Kamau.

Baada ya shule ya upili, Bi Kamau alijiunga na chuo kikuu kusomea taaluma ya Mausala ya Kigeni akiwa na nia ya kupata ajira.

Baada ya kukamilisha kozi hio, Bi Kamau aligundua kuwa bado alikuwa na hamu kuu ya kufanya kazi ya useremala.

“Niligundua kwamba hamu yangu kuu ilikuwa kutengeneza fanicha haswa viti na ndipo niliamua kujifunza kazi hiokutoka kwa mafundi mbali mbali ambao walikuwa na ujuzi wa kazi hio kwa miaka mingi ,” akasema Bi Kamau.

Parky Kamau katika karakana yake ya sofa za kisasa katika soko la Gikomba. PICHA/ MAGDALENE WANJA

Alijifunza kazi hiyo huku akifanya biashara ya kuuza nguo za mitumba ili kujipatia riziki na kujiwekea mtaji wa kuanzisha kazi yake. Baada ya miaka minne aliamua kuifanya kazi ile ambayo alihisi kuwa na msukumo wa kuifanya.

Safari yake ya ujuzi wa kutengeneza viti ilikuwa ni pamoja na kutafuta soko ambazo ziliuza mbao zenye ubora zaidi na vitambaa ambavyo vingemfaa katika kazi mbalimbali.

Hii ilifuatiwa na kuchora miundo mbalimbali ambayo ilitokana na mawazo na aliyoona mitandaoni.

“Nilipoanza kuifanya kazi hio nilijifunza kwamba kila fundi katika karakana ako na kazi yake maalum na hivyo singeweza kuifanya kazi yote bila usaidizi wa wajuzi mbali mbali,” aliongeza Bi Kamau.

Ujuzi wa kuunganisha ujulikanao ndio alijifunza kwanza ambao mwaka 2016. Hii ilifuatiwa na mafunzo zaidi katika uundaji wa viti ambazo ndio fanicha alipenda kutengeneza zaidi. Katika kazi yake ya kila siku, anafanya kazi na mafundi 15 ambao hufanya kazi mbalimbali.

Fanicha zake huuzwa kati ya Sh 12,000 na Sh 15,000. Bei hii hutegemea aina ya mbao iliyotumika kuunda bidhaa hio. Biashara hio imemuwezesha kupata faida ya Sh300,000 kwa mwezi.

“Maoni kutoka kwa wateja wangu hunisaidia sana katika kutengeneza bidhaa kuwa bora zaidi,” aliongeza Bi Kamau. Aliongeza kuwa nia yake kuu ni kuona wateja wake wameridhika kutokana na kazi yake.

You can share this post!

Walimu wote wepewe chanjo ya Covid-19 bila ubaguzi

Nakuru West Queens washinda Eldoret Falcons 3-2 ugenini