• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Magufuli bado yuko mteja

Magufuli bado yuko mteja

Na AFP

SERIKALI ya Tanzania imeendelea kukataa kusema aliko Rais John Magufuli, siku 18 baada ya kiongozi huyo kuonekana hadharani.

Badala ya kutoa majibu, utawala wa Magufuli sasa umeamua kukamata raia yeyote anayeuliza maswali kumhusu rais huyo, huku maafisa serikalini wakijitahidi kupuuza madai kwamba anaugua.

Kulingana na wachanganuzi wa masuala ya uongozi, kimya cha serikali kuhusu aliko Magufuli kina maana kuna jambo kubwa lililomtendekea.

“Ni wazi kuwa utawala wa Tanzania unachukua muda wake kuafikia lengo fulani. Serikali inapohitaji kupewa muda huwa ni aidha rais anaugua sana, hajiwezi au amefariki,” alisema mtaalamu wa masuala ya demokrasia, Prof Nic Cheeseman wa Chuo Kikuu cha Birmingham.

Mara ya mwisho Magufuli kuonekana hadharani ilikuwa Februari 27.

Licha ya kuwa muumini sugu wa Kikristo katika Kanisa Katoliki, hajahudhuria ibada kanisani kwa Jumapili tatu zilizopita. Awali ilikuwa kawaida yake kuhutubu kila wakati alipoenda kanisani.

Siku chache kabla rais kuonekana mara ya mwisho, Waziri wa Fedha Philip Mpango aliibua mjadala alipoanza kukohoa na kuonekana akikatikiwa hewa katika kikao cha wanahabari nje ya hospitali.

Waziri huyo alikuwa ameitisha kikao hicho kupuuza uvumi kwamba alikuwa amefariki baada ya kuugua Covid-19.

Kutoweka kwa Magufuli machoni pa umma kumetokea wakati ambapo kumekuwa na vifo vya watu wengi mashuhuri nchini humo. Vifo hivyo husemakana kusababishwa na ‘matatizo ya kupumua’.

Kwa miezi minne awali, Magufuli alikuwa amesisitiza hapakuwa na corona Tanzania kwa vile maombi yalifanikiwa kukomesha ugonjwa huo kuenea.

Alikataa kuvaa barakoa wala kuweka mikakati ya kupunguza maambukizi kama vile kufunga maeneo yaliyo na idadi kubwa ya maambukizi.

Nchi hiyo pia iliacha kutoa takwimu za maambukizi mnamo Aprili 2020.

Wiki moja kabla aonekane hadharani mara ya mwisho, Magufuli alikubali bado virusi vilikuwa vinaenea nchini mwake baada ya makamu wa rais wa Zanzibar kufariki kwa Covid-19.

Jumanne iliyopita, kiongozi wa upinzani Tundu Lissu, ambaye yuko mafichoni Ubelgiji, pamoja na wengine walianza kuuliza aliko Magufuli huku wakisema duru ziliwaeleza kuwa anaugua sana baada ya kuambukizwa virusi vya corona ilhali yeye huwa pia na magonjwa mengine.

Duru nyingine zimekuwa zikisema Magufuli alilazwa Nairobi kisha akapelekwa India, lakini wengine wanasema hajawahi kuondoka Tanzania.

Maafisa wa serikali ya Kenya wamekana kwamba yuko nchini, na wizara ya mashauri ya kigeni India ilikataa kujibu maswali kuhusu suala hilo.

Ijumaa iliyopita, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema Magufuli “ana nguvu na anachapa kazi kama kawaida”.

Mnamo Jumatatu, makamu wa rais Samia Suluhu alidokeza huenda rais anaugua, ingawa hakumtaja.

“Nchi yetu sasa imejaa uvumi kutoka nje lakini hayo yote yanafaa kupuuzwa…ni kawaida kwa mtu yeyote kuugua. Huu ni wakati ambao tunafaa kuungana,” akasema Suluhu.

Kiongozi wa chama pinzani cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema serikali inatoa nafasi kwa watu kuishi kwa hofu.

Mashirika ya kutetea haki yamekuwa yamekuwa yakimkashifu kwa kuhujumu demokrasia na kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari. Ni kwa msingi huu ambapo wanahabari nchini humo wanaogopa kuchunguza ukweli kuhusu aliko rais wa taifa hilo.

Kufikia sasa, polisi wanaendeleza msako dhidi ya wanaoeneza habari kuhusu afya ya Magufuli. Watu wasiopungua wanne wamekamatwa.

You can share this post!

FAUSTINE NGILA: Tuzime video feki zisivuruge uchaguzi 2022

Mutua Katuku aondolewa kwenye uwaniaji useneta Machakos