• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Mutua Katuku aondolewa kwenye uwaniaji useneta Machakos

Mutua Katuku aondolewa kwenye uwaniaji useneta Machakos

Na SAMMY WAWERU

CHAMA cha Maendeleo Chap Chap kimemwondoa mgombea wake Bw Mutua Katuku katika uchaguzi mdogo ujao wa useneta Kaunti ya Machakos.

Kiongozi wa chama hicho, Dkt Alfred Mutua amesema kimechukua hatua hiyo kutokana na uungaji wake mkono wa Handisheki na Ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

“Chama cha Maendeleo Chap Chap na ambacho kinaunga mkono Handisheki na BBI kinaamini umoja ili kuleta maendeleo na kuondoa umaskini. Tuondoe mila za siasa za utengano na anayeshinda kunyakua kila kitu…

“Maendeleo Chap Chap iliunga mkono kuchaguliwa tena kwa Rais Uhuru Kenyatta. Inanyoosha mkono wa heri njema kwa Rais na Bw Raila Odinga kwa kuondoa mwaniaji wake katika uchaguzi mdogo ujao kiti cha useneta,” akatangaza Dkt Mutua na ambaye pia ni gavana wa Machakos.

Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga walitangaza kuzika tofauti zao za kisiasa Machi 2018 kupitia salamu za maridhiano, maarufu kama Handisheki.

Ni salamu za heri njema kati ya viongozi hao ambazo zilizalisha BBI, Mswada wa marekebisho ya Katiba 2020 ambao chama cha Maendeleo Chap Chap kinaunga mkono.

Uchaguzi mdogo wa useneta Machakos na ambao Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeratibu kufanyika kesho, Alhamisi, Machi 18 ulivutia wagombea watatu wenye ushindani mkuu; Agnes Kavindu (Wiper), Mutua Katuku (Maendeleo Chap Chap) na Ulbarnus Ngengele (UDA).

Kujiondoa kwa chama hicho kwenye kinyang’anyiro, inaashiria chama cha Wiper, kinachoongozwa na Bw Kalonzo Musyoka na UDA ambacho kinahusishwa na Naibu wa Rais, Dkt William Ruto, vitapimana nguvu.

You can share this post!

Magufuli bado yuko mteja

Wakenya milioni 1.4 wanakabiliwana baa la njaa –...