• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
MAGUFULI: Mchapakazi mwenye lakabu ya ‘Bulldozer’ aliyekweza TZ

MAGUFULI: Mchapakazi mwenye lakabu ya ‘Bulldozer’ aliyekweza TZ

Na JUMA NAMLOLA

JOHN Pombe Magufuli alibatizwa jina la “Bulldozer” yaani, lile tingatinga kubwa linalotumika kuchimba mitaro au kubomoa majumba. ‘Bulldozer’ pia hutumika kwa maana ya mtu anayetumia kifua kufanikisha anayotaka.

Maana zote mbili ziliafiki vyema sifa zake. Akiwa kwenye kampeni za kutaka kuchaguliwa upya mwaka jana, Dkt Magufuli alifanya mazoezi jukwaani kuonyesha Watanzania na ulimwengu kwamba, alikuwa na nguvu na uwezo wa kuendelea kuwaongoza.

Mtindo wake wa uongozi ulikuwa kuzuru maeneo bila ya kutoa taarifa za awali na kukagua miradi ya maendeleo, hasa ujenzi wa miundomsingi. Jina la bulldozer hasa alilipata akiwa Waziri wa Ujenzi mara mbili (2000 -2006, 2010-2015) aliwakaripia wanakandarasi waliofanya kazi duni za ujenzi wa barabara.

Ingawa wapinzani wake wa kisiasa walimkashifu kwa mtindo wake wa utawala waliodai kuwa wa kiimla, aliendeleza ubuldoza wake kwa kuanzisha miradi mikuu inayoendelea Tanzania.

Mradi unaotambuliwa zaidi ni ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) itakayotumia umeme kutoka Dar es salaam kupitia Morogoro hadi Dodoma.

Huo ni umbali wa kilomita 700. Ujenzi huo wote unafadhiliwa na raslimali za Tanzania (si mkopo kutoka nje).Reli hiyo pia ina matawi ya kutoka Dar es salaam kupitia Tabora hadi Kigoma (Kilomita 1,251) na kuna inayotoka Tabora kwenda Mwanza (kilomita 379).

Kisha inayotoka Kaliua kwenda Mpanda (kilomita 210). Kwa jumla, ujenzi mzima ni kilomita 2,707, (reli ya SGR ya Kenya mara nne).Mradi wa pili ni upanuzi wa Bandari ya Dar es salaam ambapo maegesho saba yanaongezwa kina kwa kuchimbwa zaidi kutoka mita nane hadi 15.

Upanuzi huo utawezesha bandari ya Dar es salaam kushindana na ile ya Mombasa kwa kupokea meli kubwa zaidi zenye uwezo wa kubeba hata kontena 19,000.

Kuna mradi wa kilimo unaojulikana kama Mkunazi Agriculture City, mjini Zanzibar. Kupitia pesa za malipo ya uzeeni, serikali inatekeleza mradi unaolenga kuongeza uzalishaji sukari na kuzalisha kawi ya umeme kwa matumizi ya nchi nzima.

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es salaam pia ulikamilika na sasa una uwezo wa kuhudumia wateja 6.6 milioni kwa mwaka.

Tanzania pia ilijenga bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi katika bandari ya Tanga kwa ushirikiano na serikali ya Uganda. Mradi huo uliotarajiwa kukamilika mwaka jana utatumiwa kusafirisha mafuta ghafi yanayochimbwa Uganda na kuuzwa katika masoko ya kimataifa.

Ingawa Dkt Magufuli alianzisha miradi mingi, mmoja usiosahaulika ni wa awamu ya pili ya Usafiri wa Mabasi jijini Dar es salaam maarufu kama Dar es salaam Rapid Bus System (DART).

Kenya ilikuwa na mpango kama huu jijini Nairobi lakini kufikia sasa hakuna taarifa zozote kuhusu maendeleo yake. Kwenye hutoba zake, Dkt Magufuli alionekana kushikilia sera za mwanzilishi wa taifa hiyo, Julius Kambarage Nyerere, kuimarisha utaifa.Kaulimbiu yake siku zote ilikuwa NCHI YETU, UTAIFA WETU.

“Umoja na Amani ni urithi wetu Watanzania kwa mapinduzi matukufu ya Zanzibar na uhuru wetu sote. Tunapaswa kuwaenzi waasisi wa taifa letu Mwalimu J Nyerere, Baba wa Taifa hili na Hayati Amani Karume ili nchi hii izidi kusonga mbele,” iliandika Ikulu ya Tanzania, Dkt Magufuli alipokutana na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Zanziba Maalim Seif Shariff Hamad mwezi Januari mwaka huu.

You can share this post!

Magufuli hakuwa na wakati wa kuwabembeleza Wakenya

Magufuli aliiga Trump kupuuza corona