• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Magufuli hakuwa na wakati wa kuwabembeleza Wakenya

Magufuli hakuwa na wakati wa kuwabembeleza Wakenya

Na CHARLES WASONGA

MAHUSIANO ya kidiplomasia na kibiashara kati ya Kenya na Tanzania hayajakuwa mazuri chini ya utawala wa Rais John Magufuli.Wafugaji kutoka maeneo ya mpakani katika Kaunti ya Kajiado ni kati ya walioathirika zaidi na makali ya serikali ya Rais Magufuli.

Mnamo Oktoba, 2017, maafisa wa serikali ya Tanzania waliwakamata zaidi ng’ombe 1,300 wa Wakenya wa wafugaji kutoka jamii ya Wamaasai kwa kuingia nchini humo na korti ikaamua wapigwe mnada.

Licha ya serikali ya Kenya kulaani kitendo hicho na kukitaja kama kinachokwenda kinyume cha misingi ya ujirani mwema, Rais Magufuli alisisitiza kuwa serikali yake itaendelea kuwakamata mifugo watakaoingia nchini humo kutoka Kenya.’Tanzania sio shamba la kuchungia mifugo ya nchi jirani.

Ndio maana tumeamua kukamata mifugo na kuchukua hatua kwa mujibu wa kisheria, na hata huko kwao wakishika mifugo ya kutoka Tanzania wachukue hatua za kisheria za nchi hizo,’ Rais Magufuli alisisitiza.Wiki kadhaa kabla ya kitendo hicho, serikali ya Tanzania iliteketeza vifaranga 6,400 vya kuku wenye thamani ya Sh5 milioni waliokuwa wakiingizwa humo kupitia mji wa mpakani wa Namanga.

Serikali ya Tanzania ilidai kuwa kuingizwa kwa kuku hao nchini humo kungeeneza ugonjwa wa homa ya ndege.Hiyo ilikuwa ni mara ya pili, kwani awali vifaranga 5,000 walikuwa wamechomwa baada ya kukamatwa vakivukishwa kupitia mji wa Namanga.

Vile vile, maafisa wa serikali ya Tanzania wamewahi kupiga mafuruku bidhaa za maziwa kutoka Kenya na kuzuia magari ya kuwabeba watalii kuzuru mbuga za wanyama pori nchini Tanzania.

Kuanzia 2018, na baada ya visa hivyo viwili, serikali ya Tanzania iliendelea na operesheni ya kuwazuia wafanyabiashara kutoka Kenya kwa msingi kwa kile kilichotajwa kama hatua ya kulinda ushindani kibiashara.Uhusiano mbaya kati ya Kenya na Tanzania pia ulidhihirika hata baada ya Magufuli kuugua Wakenya 26 walipokamatwa nchini Tanzania.

Ilibidi Gavana wa Kajiado, Joseph Ole Lenku kulipa faini ya Sh1 milioni ili kuwanusuru Wakenya hao.Wakenya hao wlikamatwa walipovuka mpaka kupitia mji wa Illasit, Kaunti ya Kajiado kwenda kununua chakula nchini Tanzania.

Mwaka jana Tanzania ililalamika vikali kufuatia hatua ya Kenya kufunga mpaka wake na nchi hiyo kufuatia mlipuko wa Covid-19. Kenya ilichukua hatua hiyo baada ya Tanzania kukataa kuchukua hatua za kuzuia kuenea kwa maradhi hayo.

You can share this post!

Magufuli ‘alitabiri’ kifo chake Februari

MAGUFULI: Mchapakazi mwenye lakabu ya ‘Bulldozer’...