• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
ONYANGO: Magufuli alikuwa mtetezi sugu wa wanyonge halisi

ONYANGO: Magufuli alikuwa mtetezi sugu wa wanyonge halisi

Na LEONARD ONYANGO

TANGU aliyekuwa kiongozi wa Tanzania John Pombe Magufuli kufariki Jumatano, wiki iliyopita, amekuwa akimiminiwa sifa na kusutwa kwa kiwango sawa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Wakosoaji wake wanadai Magufuli alikuwa dikteta aliyekandamiza mashirika ya kijamii, uhuru wa vyombo vya habari na viongozi wa upinzani.

Kulingana na wakosoaji hao, Magufuli alitumia kifua kuendesha nchi bila kuzingatia ushauri wa watu wengine.

Ukweli ni kwamba, hapajawahi kutokea kiongozi wa nchi anayeondoka mamlakani akisifiwa na kila mtu. Hata Rais Mstaafu wa Amerika Barack Obama ambaye amekuwa akimiminiwa sifa kwa kuwa miongoni mwa viongozi bora, alikuwa na mapungufu yake.

Mgala muue haki yake mpe. Magufuli alitenda mengi mazuri kuliko mabaya.

Tofauti na viongozi wengi wa nchi za Afrika ambao hushirikiana na mabwanyenye wachache kupora rasilimali za umma, Magufuli alisimama na kupigania mamilioni ya Watanzania maskini.

Katika mataifa mengi, mabwanyenye hawa ndio hufadhili kampeni wakati wa uchaguzi na mwaniaji anaposhinda urais, inabidi arudishe fedha alizopewa kwa kuwatunuku kandarasi zote serikalini licha ya utendakazi duni.

Katika juhudi za kuboresha maisha ya Watanzania maskini, Magufuli alijitoa mhanga kukabiliana na ufisadi na kurejesha nidhamu serikalini. Watumishi wa serikali walitakiwa kuripoti afisini saa 2 asubuhi ili kuhudumia wananchi.

Humu nchini, haswa katika maeneo ya vijijini, kupata huduma katika afisi za umma ni vigumu kwani watumishi huwa wanajishughulisha na mambo yao ya kibinafsi badala ya kuhudumia wananchi.

Japo kuna taasisi huru za kukabiliana na rushwa, rais akiwa katika mstari wa mbele kukemea ufisadi, wizi wa fedha za umma utapungua kwa kiwango kikubwa – Magufuli alikuwa katika mstari wa mbele.

Kiongozi huyo pia alipiga marufuku maafisa wa serikali kuzuru mataifa ya ughaibuni kiholela ili kuzuia ufujaji wa fedha za walipa ushuru.

Magufuli alipatia kipaumbele ujenzi wa miundomsingi ambayo ni muhimu katika ustawi wa kiuchumi wa taifa lolote lile. Alisambaza umeme vijijini kwa bei nafuu.

Alipiga marufuku kampeni mikutano ya kisiasa ya mapema kabla ya uchaguzi ili kutoa mwanya kwa serikali kutekeleza miradi ya maendeleo.

Nchini Kenya, kwa mfano, wanasiasa huanza kampeni mara tu baada ya uchaguzi. Kampeni hizi hazifai kwani zinatatiza shughuli za maendeleo na kuzua taharuki nchini. Wakenya wamekuwa wakirushiana cheche za maneno ya chuki katika mitandao ya kijamii kutokana na kampeni hizi za mapema.

Magufuli aliwaleta Watanzaia elimu ya bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari.

Tangu kuingia mamlakani 2013, serikali ya Jubilee imekuwa iking’ang’ana kufanya elimu ya sekondari kuwa ya bure lakini haijafanikiwa.

Sifa za kiongozi bora ni kutetea wanyonge na wala si kutumia fursa hiyo kuwadhulumu na kujilimbikizia mali.

[email protected]

You can share this post!

WANGARI: Suluhu awe suluhu kweli kwa Tanzania na Afrika...

Pasta afokewa kupendelea vipusa