Wakili John Bwire Ajitokeza Kudhamini Mashindano ya Soka Wadi za Kaunti Ndogo Ya Taveta

NA ABDULRAHMAN SHERIFF 

VIJANA wanahitajhika kusaidiwa kuinua vipaji vya uchezaji wao ili waweze kufanikiwa kuwa wanasoka wenye vipaji vinavyohitajiwa na klabu kubwa za hapa nchini, nchi jirani na huko ng’ambo. 

Alipokuwa akizindua mashindano yake yanayohusisha klabu za wadi ya Mata katika uwanja wa Jipe, wakili John Bwire alisema kuna umuhimu wadhamini kujitokeza kuwasaidia vijana wapate kuinua vipaji vya uchezaji wao ili wapate kusajiliwa na timu kubwa hapa nchini na ng’ambo.

“Nina nia kubwa ya kuhakikisha katika kila wadi nikianzia hii ya Mata ninasaidia ili kutokee wachezaji watakaofikia viwango vya hali ya juu vya kuwawezesha kuvutia maskauti wa klabu kubwa za hapa nchini ikiwemo ile yetu ya hapa Pwani ya Bandari FC,” akasema Bwire.

Klabu 11 zinashiriki kwenye dimba hilo ambapo mshindi anatarajia kutia kibindoni Sh50,000, mshindi wa pili kutunukiwa Sh30,000 hali mshindi wa tatu kuondoka na kitita cha Sh20,000. Mbali na zawadi hizo, timu zote zinazoshiriki zitapewa seti ya jezi na mipira mitano.

Mashindano hayo ya Wakili John Bwire Cup yatafanyika wadi nyingine za kaunti hiyo ndogo ya Taveta ambapo klabu zitakazoshiriki zitanufaika na ufadhili wa wakili huyo mwenye nia ya kuhakikisha vijana wananufaika kwa njia mbalimbali kwenye mashindano yake hayo.

Katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa uwanja wa Jipe, timu ya Lakers ilianza kwa kishiindo kwa kuitandika Grigan kwa mabao 3-0. Katika mechi nyingine iliyofanyika uwanja wa Rekeke, Kimala iliifunga Rekeke FC kwa bao 1-0.

Baadhi ya maafisa wa klabu zin azoshiriki kwenye mashindano hayo wametaka wadhamini zaidi wajitokeze kuzisaidia ili ziweze kufikia viwango vya kushiriki kwenye Ligi ya Kaunti ya Taita Taveta, Ligi ya Jimbo la Pwani na Ligi za Taifa.

Habari zinazohusiana na hii