• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:50 AM
Marejeo ya Fabinho yatatupiga jeki katika gozi la UEFA dhidi ya RB Leipzig – Liverpool

Marejeo ya Fabinho yatatupiga jeki katika gozi la UEFA dhidi ya RB Leipzig – Liverpool

Na MASHIRIKA

KIUNGO raia wa Brazil, Fabinho Henrique ambaye kwa sasa anawajibishwa kama beki wa kati kambini mwa Liverpool amepona jeraha na atakuwa sehemu ya kikosi kitakachorudiana leo na RB Leipzig ya Ujerumani kwenye hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Nyota huyo raia wa Brazil amekuwa akichezeshwa na kocha Jurgen Klopp kama beki baada ya madifenda wao wakuu – Virgil van Dijk, Joel Matip na Joe Gomez kupata majeraha yanayozidi kuwaweka mkekani.

Fabinho hata hivyo aliumia tena wikendi iliyopita wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya Fulham uwanjani Anfield. Alipata jeraha hilo katika mchuano huo uliokuwa wake wa pili baada ya kuwa nje kwa mechi nne nyinginezo kutokana na jeraha la mguu alilolipata mwanzoni mwa Februari 2021.

Mechi ya kwanza kwa Fabinho kuchezea Liverpool baada ya kupona jeraha mnamo Februari ilikuwa dhidi ya Chelsea waliowakung’uta 1-0 ugani Anfield mnamo Machi 4 kabla ya Fulham kusajili matokeo sawa na hayo siku tatu baadaye.

“Kurejea kwa Fabinho ambaye atatupiga jeki kwenye safu ya ulinzi ni habari njema kwa kikosi. Tutamtegemea pakubwa ikizingatiwa kwamba beki Ozan Kabak pia anauguza jeraha la paja,” akasema kocha Jurgen Klopp.

Liverpool watashuka dimbani kunogesha kivumbi hicho kitakachochezewa jijini Budapest, Hungary wakijivunia ushindi wa 2-0 kutokana na mechi ya mkondo wa kwanza. Ushindi huo ulikuwa wao wa pili kutokana na jumla ya michuano minane iliyopita katika mashindano yote ya hadi kufikia sasa msimu huu.

“Kinyume na kampeni za EPL, tunajivunia matokeo mazuri katika UEFA. Ni matarajio yetu kwamba tutaendeleza ubabe wetu dhidi ya Leipzig na kusonga mbele kwenye kampeni za kivumbi hicho kwa mara nyingine msimu huu,” akaongeza Klopp.

Kufikia sasa, Liverpool wanakamata nafasi ya nane kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 43, saba zaidi nyuma ya Chelsea wanaofunga orodha ya nne-bora chini ya mkufunzi mpya, Thomas Tuchel aliyetimuliwa na Paris Saint-Germain (PSG) mnamo Disemba 2020.

Chini ya kocha Julian Nagelsmann, Leipzig wanalenga kufuzu kwa robo-fainali za UEFA kwa mara ya pili mfululizo baada ya kutinga nusu-fainali mnamo 2019-20.

Kikosi hicho kwa sasa kinashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa alama 53, mbili pekee nyuma ya viongozi na mabingwa watetezi Bayern Munich.

Watashuka ulingoni kuvaana leo na Liverpool wakijivunia motisha ya kushinda kila mojawapo ya mechi sita zilizopita ligini na watakosa huduma za kiungo Dominik Szoboszlai aliyesajiliwa kutoka RB Salzburg ya Austria mnamo Januari 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Badminton Kenya yapigwa marufuku baada ya mivutano ya...

Wakili John Bwire Ajitokeza Kudhamini Mashindano ya Soka...