• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
KAMAU: Raia wasihangaishwe sababu ya maendeleo

KAMAU: Raia wasihangaishwe sababu ya maendeleo

Na WANDERI KAMAU

KWA karne nyingi zilizopita, mgawiko wa kijamii katika nchi nyingi duniani umekuwa ukikitwa kwenye tofauti zilizopo kati ya watu maskini na matajiri.

Asili ya mgawiko huo inatokana na taratibu zinazotokana na mfumo wa kibepari.

Watu maskini huonekana kama wasiojiweza. Wale matajiri huwaona maskini kama watumwa wasiofaa kuwepo duniani au wanaostahili kuishi katika mazingira sawa na wanyama.

Dhana hizo dhoofu ndizo zimechangia sana mjengeko wa ubepari, hata miongoni mwa jamii ambazo hazikuwa zikiushadidia mfumo huo.

Mojawapo ya athari za ubepari ni ukosefu wa utu. Kimsingi, mabepari—kwa muktadha huu watu matajiri—hujiona kama ni wao pekee wanaopaswa kuwepo duniani.

Kwa kuongozwa na kasumba ya “kuimiliki dunia” wao hufanya kila wawezalo kumnyamazisha yeyote anayeonekana kuwa tishio kwa ushawishi wao wa kisiasa na kiuchumi.

Dhana hii ya kibepari ndiyo ilidhihirika Jumatano, wakati askari wa serikali ya Kaunti ya Kisumu walinaswa kwenye video wakimburura mchuuzi mwanamke kwa gari, kwa kisingizio cha “kukiuka kanuni za uchuuzi.”

Kwenye kisa hicho cha kusikitisha, mchuuzi huyo alijeruhiwa vibaya, huku askari hao wakionekana kutojutia kitendo chao hata kidogo.

Kama “adhabu” dhidi yao, Gavana Anyang’ Nyong’o aliwasimamisha kazi askari kwa “kuiharibia sifa” serikali yake.

Kwa yeyote aliyeshuhudia tukio hilo, kufutwa kazi si adhabu inayotosha hata kidogo kwao.

Hao ni wakiukaji wa haki za binadamu wanaopaswa kukabiliwa vikali kisheria.

Ni watu waliodhihirisha kuwa hawajali kamwe maslahi ya mwanamke aliyejituma kuwatafutia wanawe.

Hivyo, kama miongoni mwa viongozi na wasomi ambao wamekuwa wakipinga ubepari na athari zake kwa jamii, Prof Nyong’o hakufaa kuwafuta kazi tu.

Anafaa kushinikiza idara husika za kisheria kuchunguza tukio hilo na kuhakikisha waliohusika wameadhibiwa ifaavyo.

Kwenye vitabu vyake vingi, mwandishi Ngugi wa Thiong’o amekuwa akirejelea namna ujio wa dhana ya maendeleo na usasa ulivyovuruga maisha asilia ya Kiafrika.

Kulingana na serikali ya Prof Nyong’o, lengo kuu la kuwaondoa wachuuzi katikati mwa jiji la Kisumu ni kuhakikisha “linatimiza viwango vya kisasa kama jiji linalostawi kiuchumi.”

Ingawa maendeleo ni suala nzuri na la manufaa kwa jamii, maswali yanayoibuka ni ikiwa yanapaswa kutekelezwa kwa kuvuruga maisha ya wenyeji.

Kando na Kisumu, maelfu ya Wakenya wamepoteza mali ya mamilioni ya pesa baada ya kubomolewa nyumba zao ili “kubuni nafasi” kwa ujenzi wa reli ya kisasa.

Si Nairobi, Nyeri au Nakuru—vilio vya Wakenya vilisikika kotekote wakiirai serikali kuwapa muda kuokoa mali yao.

Kama Shetani au Izraili Malaika wa Kifo, matinga yasio huruma yaliviangukia vibanda na nyumba zao bila huruma.

Kwa muda wa dakika chache tu, maeneo yaliyokuwa yamejaa makazi na biashara za watu yaligeuka kuwa kama nyanja za kuchezea mpira. Hakuna hata jengo moja lililobaki. Yote yaliangushwa na kugeuka magae tu.

Imani yangu ni kuwa si namna hii ambayo maendeleo yanapaswa kuendeshwa. Wananchi pia wana haki ambazo lazima ziheshimiwe na kuzingatiwa.

[email protected]

You can share this post!

MATHEKA: Wimbi la tatu la corona lachangiwa zaidi na...

Dkt Ruto akiungana na Raila, kipi kitarajiwe Mlima Kenya...