• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:19 PM
Dkt Ruto akiungana na Raila, kipi kitarajiwe Mlima Kenya 2022?

Dkt Ruto akiungana na Raila, kipi kitarajiwe Mlima Kenya 2022?

Na MWANGI MUIRURI

HABARI kuwa Naibu Rais Dkt William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga wanaweza wakaungana kusaka urais katika uchaguzi mkuu wa 2022 zimezua hisia mseto Mlima Kenya.

Hofu ni kuwa, ikiwa hilo litafanyika, eneo hilo ambalo limekuwa katika uongozi wa taifa hili katika serikali tatu tangu uhuru (Hayati Mzee Jomo Kenyatta 1963-1978, Mwai Kibaki 2002-2013 na Uhuru Kenyatta 2013 hadi sasa) litatengwa na lijipate katika upinzani.

Mchanganuzi wa kisiasa Bw Gasper Odhiambo anasema Dkt Ruto akiungana na Bw Odinga, basi itakuwa ni njia ya uhakika ya kuadhibu upande wa Rais Kenyatta iwapo kiongozi wa nchi atasaliti ahidi ya ‘Yangu Kumi na ya Ruto Kumi’.

“Ni hali inayoweza kuitupa jamii ya Rais katika pipa la giza kisiasa,” asema Bw Odhiambo.

Hata hivyo, anasema muungano wa Dkt Ruto na Bw Odinga unaweza ukasambaratishwa na Mlima Kenya nao wakiamua kujipanga upya na kusaka muungano wao kwa kuwa naye Bw Odinga anatengwa na Musalia Mudavadi wa ANC, Kalonzo Musyoka wa Wiper, Moses Wetang’ula wa Ford Kenya na Gideon Moi wa Kanu.

“Ukiangalia mpangilo huo, utapata kwamba Dkt Ruto na Bw Odinga wakiungana halafu Mlima Kenya ijitenge nao kabisa, basi huenda wasifaulu,” asema.

Anasema kuwa ule muungano hatari kwa Mlima Kenya ni ule ambao utawaleta pamoja Mudavadi, Kalonzo, Moi na Wetang’ula kisha Bw Odinga na Dkt Ruto waungane nao akisema kuwa hali kama hiyo itawaacha wapigakura wa Mlima Kenya wakiwa peke yao dhidi ya Wakenya wengine wote.

“Hao wote wakija pamoja dhidi ya Mlima Kenya na wapate mbinu ya kukubaliana kuhusu mwaniaji mmoja ambaye atakuwa ama Dkt Ruto au Bw Odinga na hawa wengine wote watii, basi hapo ndipo taharuki ya Gema kutengwa itaibuka, lakini sio katika hali nyingine yoyote ya miungano,” aeleza.

Hata hivyo, walio katika mrengo wa ‘Tangatanga’ ambao hufuata Dkt Ruto wamepuuzilia mbali muungano huo wakisema hata ukiibuka na utekelezwe, kile kitafanyika hakitaathiri uwezo wa Mlima Kenya kuwa ndani ya serikali.

“Habari hizo zilitokana na mahojiano ya Dkt Ruto na kituo cha Radio Citizen ambapo alikuwa muwazi kwamba ikiwa ataungana na Bw Odinga, itakuwa ni ODM ije ndani ya ‘Tangatanga’ wala sio sisi tuwaendee. Ina maana kuwa atakuja kwa masharti yetu,” akasema Mbunge wa Mathira Bw Rigathi Gachagua.

Bw Gachagua anasema kuwa msimamo wa ‘Tangatanga’ ni kuwa hata muungano wa kisiasa uwe wa nani kati ya mwingine nani au chama gani na kingine kipi, ni lazima iwe Dkt Ruto ndiye atakuwa mgombea wa urais.

Ikiwa Bw Odinga atajiunga na Dkt Ruto basi “aridhike na nafasi ya Waziri Mkuu na hilo itabidi kwanza BBI ipitishwe katika referenda na kisha awanie ubunge, ashinde ndipo ateuliwe kuwa Waziri Mkuu.”

Pendekezo la wadhifa wa Waziri Mkuu katika BBI ni kwamba atakayeteuliwa ni lazima awe mbunge.

Bw Gachagua alisema kuwa ikiwa Dkt Ruto ataingia kwa muungano wa kisiasa na Bw Odinga na akubali kutowania urais (Dkt Ruto) “basi sisi tutajitoa na tupange upya mikakati yetu ya kisiasa kwa kuwa Bw Odinga kamwe hawezi kuwa chaguo letu la kisiasa na hakuna vile tutamuunga mkono kama Mlima Kenya ndio awe rais.”

Seneta wa Murang’a Bw Irungu Kang’ata alisema huo muungano unaosemwa sio mbaya ila tu eneo la Mlima Kenya “limeamua kuwa mwaniaji wao wa urais ni Dkt Ruto wala sio mwingine yeyote na ikiwa hilo litasambaratika kupitia mikakati yoyote ile itaibuka katika miungano ya kisiasa, basi tuko tayari kuanza kujipanga upya.”

Aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Peter Kenneth alisema kuwa uwezekano huo wa Dkt Ruto na Bw Odinga ni kiini cha kuwatuma wanasiasa wote wa Mlima Kenya kwanza waungane na wapange mikakati yao ya 2022 wakielewa kuwa “hata kina nani waungane Kenya hii, sisi tukiwa na umoja wetu wa kura na tukatae katakata kuzigawa katika debe, tutawatatiza pakubwa.”

Alisema kuwa hali ya siasa ni sawa na jinsi mto mkubwa hupewa maji na mito midogo katika safari ya kujaza bahari.

“Hii ina maana kuwa sisi kama walio na asilimia 35 ya kura zote hapa nchini, ikiwa tunatumbukiza katika kapu moja kisiasa, tunahitaji tu asilimia 16 ya nyongeza ya kura ili tuibuke na ushindi. Hakuna sheria imeundwa Kenya hii ya kutuzuilia kuwania urais na ikiwa mito midogo hupea maji mto mkubwa, hata wakiungana, kinga yetu ni umoja wetu,” akasema Bw Kenneth.

Bw Kenneth alisema kuna haja kubwa ya wanasiasa wa Mlima Kenya sasa kutupilia mbali tofauti zao na kwanza wavunje mirengo yao hasidi ya kisiasa na cha maana kama hali ya dharura, waungane na waanze kuongea kwa sauti moja ili uzito wao wa kura utambulike na uheshimiwe.

Alisema kuwa “tukiungana, liwe liwalo tutakuwa ndani ya serikali ya baada ya 2022 tukiwakilishwa na mtu wa eneo hili ama katika wadhifa wa rais, naibu wa rais au waziri mkuu.”

Kwa mujibu wa Seneta wa Nyeri Ephraim Maina, “nimekuwa nikionya kuwa tunapelekwa mbio isiyofaa na baadhi ya wanasiasa wetu ambao tangu 2013 wamekuwa wakituchuuza kwa mirengo fulani ya kisiasa bila kuzingatia athari za kutokuwa na subira darubini ya kisawasawa ipigwe kujua tunaelekezwa wapi na ni wapi kunatufaa zaidi.”

“Rais Kenyatta amekuwa akihofia hilo la kutengwa kufanyika na ndipo amekuwa akisisitiza umuhimu wa BBI ambayo inaunda serikali pana inayojumuisha maeneo hapa nchini kulingana na kura zao na kisha kugawa rasilimali kulingana na idadi ya watu,” akasema Bw Maina.

Bw Maina ameambia Taifa Leo “hii ndiyo hali ambayo Rais amekuwa akijaribu kuzima na ndiyo hali wale ambao wanatuchuuza kwa mrengo wa Dkt Ruto wamekuwa wakipinga bila kuzingatia kwamba kiongozi wa nchi huwa na ufahamu zaidi wa mitindo na njama za wanasiasa kupitia habari za ujasusi.”

Akasema: “Rais alijua haya yalikuwa na uwezekano wa kutokea na ndipo akazindua mpango wa kuhakikisha eneo la Mlima Kenya huwa linapangiwa njama za kulitenga kisiasa kutokana na wingi wa kura zao na mtindo wao wa kupendelea mwaniaji wao katika uchaguzi wa urais.”

Aliyekuwa mbunge wa Maragua Bw Elias Mbau naye akasema kuwa “sasa ni wazi kuwa busara ya Rais Kenyatta ya kuwataka watu wa Mlima Kenya waunge mkono mchakato wa BBI ilikuwa na kiini cha kumulika uwezekano wa kutengwa kwa Mlima Kenya.”

Hata hivyo, mchanganuzi wa kisiasa Prof Ngugi Njoroge anauliza: “Hili la kutiwa hofu kuwa huenda Mlima Kenya wakatengwa kisiasa na waingie upinzani lina mashiko kweli? Kuna ushahidi kuwa wapigakura wa eneo hilo wana tamaa ya kuwa ndani ya serikali?”

Anauliza pia: “Wakati wenyeji wa Mlima Kenya walianza kuonyesha nia ya kuunga mkono mwingine katika wadhifa wa urais 2022, ilikuwa ni ishara kuwa wamechoka kuhusishwa na serikali haswa baada ya kuibuka kuwa wadhifa huo huwa hauwasaidii sana kumaliza shida zao?”

Anasema kuwa hata miungano iundwe kwa msingi upi, Wakenya watafanya maamuzi yao “na sioni ule msukumo mkubwa wa jadi Mlima Kenya wa kupambana kufa kupona kuwa ndani ya serikali kama upo kwa sasa.”

“Wenyeji wamechoka kujumuishwa ndani ya ukabila wa kuwindia mtu binafsi ukubwa na hatimaye kuachwa kwa mataa kila mmoja wao akipambana na hali yake,” akasema.

You can share this post!

KAMAU: Raia wasihangaishwe sababu ya maendeleo

Ibrahimovic atambisha Uswidi katika mechi ya kwanza tangu...