• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
Suluhu atoa hongera kwa raia kwa uzalendo mkuu

Suluhu atoa hongera kwa raia kwa uzalendo mkuu

Na MWANANCHI

DAR ES SALAAM, Tanzania

RAIS Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, ameyashukuru makundi mbalimbali kwa kusimama na serikali tangu kutangazwa kwa kifo cha mtangulizi wake, John Magufuli.

“Leo (jana Ijumaa) tunapompumzisha mpendwa wetu Hayati Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli, kwa niaba yangu binafsi na niaba ya watu na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nataka kuwashukuru Watanzania wenzangu, viongozi wenzangu pamoja na viongozi wastaafu. Viongozi wa nchi na mashirika mbalimbali ya kimataifa, viongozi wa dini, siasa, wanadiplomasia, wanahabari, wasanii na kila aliyekuwa nasi bega kwa bega wakati huu mgumu kwa taifa letu. Tafadhali pokeeni shukrani zetu za dhati na muendelee kuiombea roho ya Dkt Magufuli ipumzike kwa amani na Mungu aendelee kuifariji familia yake,” akasema.

Wasanii wa Tanzania walionyesha uzalendo wa hali ya juu kwa kuungana kutunga na kuimba nyimbo za kumuomboleza Magufuli, wakimsifu kwa miradi ya maendeleo, vita dhidi ya ufisadi na kuhimiza uwajibikaji katika serikali.

Mbunge wa zamani wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alisema atamkumbuka Magufuli kwa mambo makubwa matatu.

Mchungaji Msigwa, ambaye Ijumaa aliungana na mamia ya watu mjini Chato, Mkoa wa Geita katika mazishi ya Magufuli, aliyataja mambo hayo kuwa ni kurejesha nidhamu kazini, uwajibikaji na uthubutu.

Katika uwanja wa Magufuli ilikofanyika ibada ya mazishi, viongozi na wananchi waliwasili kwa wingi kumuaga Magufuli.

Magufuli alifariki mnamo Machi 18 akitibiwa maradhi ya moyo katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 61.

Rais Suluhu, aliyekuwa makamu rais, aliapishwa rais baadaye kulingana na katiba ya Tanzania.

You can share this post!

Wakurugenzi wa shirika la KTDA wakataa kutuliza boli

TAHARIRI: Heko kwa Harambee Stars kujikaza kisabuni