• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
KAMAU: Sakata ya KCPE ishara uozo bado upo Wizara ya Elimu

KAMAU: Sakata ya KCPE ishara uozo bado upo Wizara ya Elimu

Na WANDERI KAMAU

LENGO kuu la mfumo wowote wa elimu ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wanafaidika kwa ujuzi ambao utawafaa baadaye maishani.

Hiyo ndiyo imekuwa azma ya mageuzi mbalimbali ambayo yamekuwa yakifanyiwa mifumo ya elimu nchini tangu tulipojinyakulia uhuru.

Vile vile, ndilo lengo la mageuzi yanayoendelea kwa sasa, ambapo serikali imekumbatia Mfumo wa Elimu Tekelezi (CBC) kama ulio bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Mfumo wa 8-4-4 tunaoutumia kwa sasa umelaumiwa kwa kutilia maanani matokeo ya wanafunzi kwenye mitihani ya kitaifa badala ya mafunzo wanayopata, tangu kuzinduliwa kwake mnamo 1985.

Mkazo huo umekosolewa kwa kujenga dhana isiyofaa miongoni mwa wanafunzi; kwamba lazima wapite mtihani kufaulu maishani.

Taharuki hiyo ndiyo imekuwa ikifanya baadhi ya wakuu wa shule za kibinafsi kufanya kila wawezalo kuhakikisha shule zao zinafanya vyema kwenye mitihani ya kitaifa ya Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE).

Mfano ni sakata ambayo imeibuka kuhusu mtihani wa KCPE uliokamilika majuzi, kwamba kulikuwa na njama kuhusu ujumuishaji wa baadhi ya maswali kwenye mtihani huo.

Inakisiwa baadhi ya shule za kibinafsi “zilinunua” mtihani huo kabla yake kuanza rasmi nchini.

Inadaiwa njama hizo ziliendeshwa na baadhi ya maafisa wa elimu kwa ushirikiano na wamiliki wa shule za kibinafsi za hadhi.

Ingawa Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, alikana madai hayo jana, ni wazi kuwa wizi wa mitihani bado ni saratani ambayo inaendelea kuathiri sekta na ubora wa elimu nchini kwa jumla.

Alipohudumu kama Waziri wa Elimu kati ya 2013 na 2018, Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, alijaribu awezavyo kuvunja mitandao ya watu walaghai, ambao walikuwa wakitumia ushawishi wao kutekeleza udanganyifu wa mitihani ya kitaifa.

Mitandao hiyo ilijumuisha maafisa wa wizara pamoja na shule za kibinafsi na umma. Juhudi zake zilifaulu.

Hata hivyo, inasikitisha kuwa saratani hiyo imerejea tena; na kwa ukali unaotishia kuvuruga mafanikio yote yaliyokuwa yamepatikana kwenye juhudi za kumaliza udanganyifu wa mitihani ya kitaifa.

Wito wetu ni kwa Prof Magoha kufuata nyayo za Dkt Matiang’i; kuvunjavunja mitandao hiyo au kuwafuta kazi maafisa ambao watapatikana kushiriki sakata hizo.

Semi kali hazitasaidia kwa vyovyote vile. Hatua kali ndizo zitaokoa kizazi cha sasa dhidi ya majuto ya baadaye maishani mwao.

[email protected]

You can share this post!

MUTUA: Suluhu aponye madonda aliyoacha Rais Magufuli

UoN yafungwa