• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Pasaka ya hasara kwa wamiliki hoteli Pwani

Pasaka ya hasara kwa wamiliki hoteli Pwani

Na KALUME KAZUNGU

SEKTA ya utalii ukanda wa Pwani imepata pigo jingine wakati ambapo wenye hoteli sasa wanakimbilia kuzifunga hoteli zao kwa kushindwa kustahimili masharti makali yaliyowekwa na serikali kudhibiti janga la corona.

Juma lililopita, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza marufuku ya kuingia na kutoka kwenye kaunti tano, ikiwemo Nairobi, Kiambu, Machakos, Kajiado na Nakuru.

Cha kusikitisha ni kwamba kaunti hizo tano zilizofungwa ndizo zinazotoa watalii wengi wa ndani kwa ndani na wale wa kimataifa wanaozuru Pwani ya Kenya kujivinjari kila mara.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo mwishoni mwa juma, ambapo watalii wengi walitarajiwa kufurika kwenye sehemu mbalimbali za burudani na hoteli kuadhimisha Pasaka ulibaini kuwa hoteli nyingi zilibaki ukiwa.

Baadhi ya wenye mahoteli waliozungumza na Taifa Leo walisema wameafikia kufunga hoteli zao na kuwatuma wafanyakazi wao nyumbani hadi pale hali shwari itakaporejelewa nchini.

Wamiliki wa hoteli za kifahari eneo la Lamu, ikiwemo Majlis na Peponi kwenye eneo la Shella na Lamu House, Lamu Palace na Sunsail zilizoko kisiwa cha Lamu, walikiri kupokea asilimia zaidi ya 90 ya maombi ya wageni kukatiza safari zao kufuatia marufuku ya kutotoka au kuingia kwenye kaunti tano zilizotajwa.

Mmiliki wa hoteli ya kifahari ya Peponi eneo la Shella, kisiwani Lamu, Bi Carol Korschen alisema wameafikia kuifunga hoteli hiyo na kuwatuma nyumbani wafanyakazi wake 125 hadi pale mahangaiko ya Covid-19 yatakapokoma.

Kwa mujibu wa Bi Korschen, hoteli ya Peponi iko na vyumba 28 lakini kufikia Ijumaa, Jumamosi na Jumapili ambapo Pasaka ilikuwa ikiadhimishwa, ni wageni 9 pekee waliokuwa wamekodi vyumba hotelini humo.

“Usimamizi wa hoteli hii umepanga kuifunga hoteli kufikia Aprili 6 mwaka huu. Hii ni kutokana na uhaba wa wageni wanaozuru hotelini kwa sasa. Fedha za kukimu mahitaji ya hoteli, ikiwemo kulipa wafanyakazi hakuna. Biashara imedidimia. Tutafunga hoteli ili kuwapa nafasi wafanyakazi wangu 125 kwenda nyumbani kukutana na familia zao na kuepuka kuambukizwa corona. Tutafungua hoteli wakati ambapo mafuruku nyingi za corona zitakuwa zimeondolewa nchini,” akasema Bi Korschen.

Katika hoteli ya kifahari ya Majlis ambayo pia iko eneo la Shella, mmoja wa maafisa wanaosimamia hoteli hiyo na ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema kufikia Jumapili, ni chumba kimoja pekee kati ya vyumba 40 vilivyoko hotelini humo ambacho kilikuwa kimekodishwa.

Afisa huyo msimamizi alisema kutokana na uhaba wa watalii na wageni wanozuru hotelini humo, usimamizi wa hoteli uliafikia kupunguza idadi ya wafanyakazi kwa asilimia 35.

“Tuko na zaidi ya wafanyakazi 100 hotelini hapa. Watalii na wageni hawazuru tena Lamu kutokana na marufuku ya kuingia na kutoka kaunti tano za Kenya. Tayari tumepunguza idadi ya wafanyakazi. Isitoshe, hata wale waliobaki pia tumewapunguzia mishahara ili kuwezesha hoteli yetu kuendelea,” akasema afisa huyo.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadau wa Utalii, Kaunti ya Lamu, Abdallah Fadhil, alimuomba Rais Uhuru Kenyatta kuondoa mafuruku ya kuingia na kutoka kwenye kaunti tano,

akizitaja kaunti hizo kuwa muhimu kwa uendelezaji wa sekta ya utalii kaunti ya Lamu na Pwani kwa jumla.

“Sisi hapa Lamu hutegemea sana watalii kutoka Nairobi, Machakos, Kiambu, Kajiado na Nakuru. Cha kusikitisha ni kwamba serikali imezifunga kaunti hizo. Hii inamaanisha hatuna watalii wanaozuru Lamu kwa sasa. Hoteli nyingi tayari zimefungwa. Ningemuomba Rais Kenyatta kutuonea imani na kuzifungua kaunti tano ili kufufua sekta yetu ya utalii hapa Lamu na Pwani kwa jumla,” akasema Bw Fadhil.

Kwa upande wake, Waziri wa Utalii, Biashara na Maendeleo ya kiviwanda, Josephat Musembi, alisema serikali ya kaunti ya Lamu ina mpango wa kukutana na wadau wa sekta zote kuu za Lamu, ikiwemo utalii, hoteli, biashara na hata uvuvi ili kujadili na kutahmini hali katika hatua ya kupiga jeki utalii wa eneo hilo.

“Tunakutana washikadau wote juma lijalo. Tunataka kujadili suala hili la utalii, biashara na uvuvi ili kujua ni wapi kutahitaji usaidizi zaidi wakati huu ambapo serikali inapigana na janga la Covid-19,” akasema Bw Musembi.

You can share this post!

Kivumbi kikali chaja, wandani wa Gideon waonya mahasimu

Watalii wafurika kupokea chanjo wenyeji wakisusia