• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:30 PM
Wachuuzi wa vyakula Ruiru walalamika

Wachuuzi wa vyakula Ruiru walalamika

Na LAWRENCE ONGARO

WACHUUZI wanaouza vyakula mjini Ruiru waliandamana mwishoni wiki jana kwa kile walichotaja kama kudhulumiwa na askari wa Kaunti ya Kiambu.

Walidai ya kwamba askari hao waliwafurusha kuondoka kando ya barabara katika eneo la masoko na majengo mjini Ruiru.

Bw Peter Ngige ambaye huuza matunda katika eneo hilo alisema waliharibu mali yao huku wakifurushwa kutoka maeneo hayo.

“Sisi kama wachuuzi wa hapa kwa muda mrefu tumeshangaa kuona ya kwamba kaunti ya Kiambu haina huruma na inatumia nguvu kupita kiasi dhidi ya wachuuzi wa Ruiru. Wanawapiga watu bila huruma huku wakivunja vibanda vyetu,” alisema Bw Ngige.

Bi Jane Kireya alisema amekuwa akiuza mboga na nyanya tangu mwaka wa 2016 na ni vibaya wao kutuvamia ghafla bila kutupatia ilani.

“Sisi wachuuzi wa vyakula tulipata hasara kubwa kwani bidhaa zetu zilitawanywa na nyingine kuchukuliwa kwa nguvu,” alisema Bi Kireya.

Alisema ni vyema gavana James Nyoro kuingilia kati jambo hilo kwa sababu hawana njia nyingine ya kupata riziki yao ya kila siku.

“Mimi nina watoto ambao wananitegemea na sasa sijui nitafanya nini na nitalilia nani anisaidie,” alijitetea Bi Kireya.

Bi Mary Wangari alisema mboga na nyanya anazouza zilitawanywa kila mahali huku akitishwa kupiga kwa rungu.

“Sisi kama wafanyabiashara wadogowadogo ni lazima tulindwe ili tusiendelee kunyanyaswa. Tuko na familia zinazotutegemea na kwa hivyo mazungumzo ni muhimu badala ya fujo,” alisema Bi Wangari.

Biashara nyingi mjini Ruiru zilisimamishwa kwa sababu ya vurugu iliyokuwepo kwa zaidi ya muda wa saa tatu hivi.

Juhudi za kutafuta maafisa wakuu wa kaunti ya Kiambu ziligonga mwamba kwani hawakupatikana kwa simu.

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Tohara yazua utata ikiwa ifanywe kitamaduni...

Wakiukaji 1,600 wa masharti ya corona wanaswa...