• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Inter Milan yaanza kunusia taji la Serie A

Inter Milan yaanza kunusia taji la Serie A

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI matata wa inter Milan, Romelu Lukaku, alifunga bao la pekee katika ushindi muhimu wa ugenini dhidi ya Bologna, na kuiwezesha timu yake kufungua zaidi mwanya kileleni mwa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo Jumamosi.

Ni ushindi uliosaidia masogora hao wa kocha Antonio Conte kuanza kunusia taji lao la kwanza la Serie A tangu msimu wa 2009-10; ikizingatiwa kuwa washindani wao wakuu AC Milan na Juventus walijikwaa katika mechi zao.

Mabingwa watetezi Juventus waliambulia sare ya 2-2 dhidi ya Torino ugenini, huku AC Milan ikikabwa koo kwa sare ya 1-1 dhidi ya Sampdoria uwanjani San Siro.

Inter kwa sasa wanaselelea kileleni mwa Serie A kwa alama 68, nane zaidi kuliko nambari mbili AC Milan.

Atalanta wanakamata nafasi ya tatu kwa pointi 58, mbili kuliko Juventus wanaofunga orodha ya nne-bora.

Nafuu zaidi kwa Inter ni kwamba wana mchuano wa akiba ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimetandazwa na Milan na Atalanta, ambazo zimepiga 29 kila mmoja.

Lukaku alicheka na nyavu za wenyeji wao dakika ya 31 baada ya jaribio la awali la mpira wa kichwa kudhibitiwa vilivyo na kipa Federico Ravaglia.

Fowadi huyo wa zamani wa Chelsea, Everton na Manchester United sasa anajivunia jumla ya mabao 20 katika mechi 28 ambazo zimetandazwa na Inter ligini.

Idadi hiyo ya magoli inamweka katika nafasi ya pili, nyuma ya Cristiano Ronaldo wa Juventus, katika orodha ya wafungaji bora wa Serie A kufikia sasa msimu huu. Ronaldo amefuma nyavu za wapinzani mara 24.

Luis Muriel wa Atalanta anashikilia nafasi ya tatu kwa mabao 18, matatu zaidi kuliko Simeon Nwankwo wa Crotone, ambao wanavuta mkia wa jedwali la Serie A kwa alama 15 kutokana na mechi 29 zilizopita.

Inter waliwalemea Bologna katika takriban kila idara huku Lautaro Martinez akishuhudia kombora lake likibusu mwamba wa goli kunako dakika ya 50.

Katika debi ya Turin iliyokutanisha masogora wa kocha Andrea Pirlo na Torino, mvamizi Federico Chiesa aliwafungulia Juventus ukurasa wa mabao katika dakika ya 13 kabla ya Antonio Sanabria kusawazisha dakika 14 baadaye.

Sanabria kisha aliwaweka Torino kifua mbele sekunde 13 baada ya kipindi cha pili kuanza, kabla ya Ronaldo kuvunia Juventus alama moja muhimu katika dakika ya 79.

Matokeo hayo yaliwasaza Torino katika nafasi ya 17 kwa alama 24, mbili pekee mbele ya Cagliari ambao kwa pamoja na Parma na Crotone wanakodolea macho hatari ya kuteremshwa ngazi mwishoni mwa msimu huu.

Torino kwa sasa wamesakata jumla ya michuano 14 bila ya kushinda Juventus, ambao ni watani wao wakubwa jijini Turin.

Chini ya kocha Stefano Pioli, AC Milan walifunga bao la kusawazisha dhidi ya Sampdoria katika dakika ya 87 kupitia Jens Petter Hauge, aliyetokea benchi kipindi cha pili.

Sampdoria, ambao waliwekwa uongozini na Fabio Quagliarella kunako dakika ya 57, walikamilisha mechi wakiwa wachezaji 10 uwanjani baada ya Adrien Silva kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 59.

You can share this post!

Mvamizi Hassan analenga magoli yasiyopungua 15 kikosini...

Hii ni aibu! Kocha Arteta achemka baada ya kichapo cha...