• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
VITUKO: Bawabu amgeuzia mwalimu mkuu kibao cha wizi wa nafaka

VITUKO: Bawabu amgeuzia mwalimu mkuu kibao cha wizi wa nafaka

Na SAMUEL SHIUNDU

SIMBAMWENE aliifahamu kazi yake vyema.

Hakuwa mgeni katika shughuli ya kuendesha mitihani ya kitaifa. Licha ya tajiriba hii pevu ya kuraukia kuchukua karatasi za mitihani katika makao makuu ya elimu wilayani na kuzirejesha jioni baada ya mtihani kukamilika, hakuwahi kusimamia mitihani nyakati za pasaka.

Kutokana na hali hii mpya, mwalimu huyu mkuu wa Bushiangala alijipata karauka Jumatatu ya pasaka ili awahi makao makuu ya elimu.

“Leo umeraukia ibada mapema sana mwalimu. Nadhani hata malango ya parokia hayajafunguliwa. “jirani yake mmoja alimjuza. “Kweli Corona imewakumbusha walimwengu kumhusu Mungu. Siamini kama wewe ni Simba uliyerauka hivi kwenda kuadhimisha ufufuko wa Yesu.” Jirani mwingine aliongeza.

Maneno ya majirani yalimzindua. Yakamkumbusha kuwa Jumatatu hiyo ilikuwa siku kuu. Alitaka kurejea ndani akakipumzishe kiwiliwili chake kilichokusanya mavune ya wiki sasa tangu mitihani ing’oe nanga lakini akaghairi nia. Hakutaka majirani wagundue kuwa alikuwa karaukia kuiendea mitihani siku kuu. Akaamua kufika shuleni kisha afike mangweni kwa Nafoyo.

Alichokipata shuleni kilimshtua. Alimfumania bawabu wa shule akifungasha nafaka ili aondoke nayo. Aliyefumaniwa alianguka miguuni pa mwalimu Simba na kuomba msamaha. “Tafadhali usinipeleke mbele. Naomba yaishie hapa. Sitarudia tena.” Alisihi.

Simbamwene alimhurumia yule mzee aliyenyenyekea miguuni pake. Akamsamehe na kuelekea kwa Nafoyo ili apumzishe akili. Huko aliwapata wateja wenzake wakibugia makopo ya kangara. Akapewa lake na kukaa faraghani na Sindwele. Huko faraghani, akamsimulia mwenzake kisa cha bawabu aliyemfumania akiiba mahindi na maharagwe kwenye stoo ya shule.

“Ulikosea kumsamehe. Huko kujaribisha wizi ni mzaha unaoweza kusababisha usaha. Mkunje angali mbichi asije akazoea.” Sindwele aliusia.

Alisisitiza kuwa bawabu huyo alipaswa kuchukuliwa hatua ili ashikishwe adabu na labda atoe kitu kidogo au awanunulie kinywaji. Simba akaafikiana na Sindwele na akampeleka bawabu kwa menyekiti wa halmashauri ya shule.

Bawabu aliposomewa mashtaka na mwenyekiti wa bodi ya shule, aliomba ruhusa ya kumuuliza Simba maswali. Akakubaliwa. “Mwalimu, kazi yangu ni ya mchana au usiku?”

“Usiku” Simba akajibu.

“Na yako ni ya mchana au usiku?”

“Mchana bila shaka.” Simba alianza kuchukizwa na maswali ya bawabu.

“Sasa basi shuleni ulifwata nini usiku. Huoni kama ni mimi nilikufumania ukiiba na sasa unanisingizia ili ujiondoe lawamani?” bawabu alimuuliza Simba.

Simba aliemewa. Hakutarajia mambo kuchukua mkondo huo. Kengele ikalia kuashiria mwisho wa mitihani ya siku. Kikao kikafungwa hadi wiki ijayo ambapo mwenyekiti angetoa uamuzi.

You can share this post!

Afisa wa GSU amuua mkewe kisha naye ajitoa uhai

Matokeo ya KCPE kutolewa mwezi huu