• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 1:15 PM
TAHARIRI: Huduma za polisi zijumuishe ushauri

TAHARIRI: Huduma za polisi zijumuishe ushauri

KITENGO CHA UHARIRI

MAUAJI yanayoendelezwa na maafisa wa usalama yamefikia kiwango cha kutisha.

Mbali na wanaochukua hatua ya kujimaliza, wapo ambao wameripotiwa kuwashambulia watu na kuwaua kutokana na sababu zisizokuwa za msingi.

Wiki hii pekee kuna visa kadhaa vya matukio ya aina hiyo. Katika Kaunti ya Baringo, kuna kisa cha afisa wa polisi aliyekamatwa kwa madai ya kumuua mmiliki wa baa. Inadaiwa kuwa mwendo wa saa saba za usiku, afisa huyo badala ya kutimiza kanuni za kafyu, aliamua kulewa na wenzake na alipoitishwa Sh450, akamgeukia mwenye baa na kumdunga kwa kisu.

Siku hiyo hiyo, afisa mwingine alikuwa amejiua katika eneo la Ruaraka, Nairobi baada ya kumuua mkewe kwa risasi. Mke huyo pia alikuwa afisa wa polisi.

Matukio haya mawili yanaibua maswali mengi kuhusiana na utendakazi wa polisi, kazi ya Tume ya Huduma za Polisi (NPSC) na wajibu wa maafisa hao katika utekelezaji wa maagizo ya serikali, ikiwemo kafyu.

Maafisa wa usalama wana jukumu la kufuata amri. Mojawapo ya amri hizo ni ile ya Rais Uhuru Kenyatta aliyoitoa wiki mbili zilizopita kuhusu kafyu. Ingawa polisi huonekana kutekeleza kanuni hizo katikati ya miji, hali ni tofauti viungani na kwenye miji midogo. Hata Nairobi, kuna mitaa ambapo maafisa hao wakiwa kwenye magari ya polisi, hupita na kukusanya ‘ushuru’ kisha huungana na wateha wengine kulewa hadi usiku wa manane.

Huu ni utovu wa nidhamu. Utovu huo hauwezi kuendelezwa bila ya maafisa wanaowasimamia kuwa na habari. Inawezekanaje afisa aliyetumwa kuzuia watu kutangatanga mitaani, kuhakikisha baa zinafungwa kufikia saa moja usiku, akae baa na kulewa hadi saa saba?

Wengine huchukua hatua ya kuua kwa jambo dogo tu. Masuala ya ndoa yanahitaji uvumilivu na kuzungumza. Si polisi peke yao ambao ndoa zao zina misukosuko au wanakumbana na mambo yanayowaudhi.

Kuchukua sheria mikononi kunaonyesha hawafunzwi ipasavyo chuoni, au wanafanya kazi katika mazingira yanayowafanya wawe na msongo wa mawazo.

NPSC yapaswa kuangalia upya huduma za kiafya za polisi, hasa ushauri wa kisaikolojia. Wengi hutumwa maeneo ya ajali, kwenye ghasia au vita na hukumbana na matukio yanayowaathiri akili. Polisi ni binadamu. Matukio hayo huwatatiza kiakili na hayawezi kuwapa utulivu bila ya ushauri nasaha.

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Vijana 2 wanaotengeneza mafuta kutokana na...

KINYUA BIN KING’ORI: ODM, Raila watajilaumu wenyewe...