• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 4:43 PM
MAKALA MAALUM: Vijana 2 wanaotengeneza mafuta kutokana na karatasi za plastiki

MAKALA MAALUM: Vijana 2 wanaotengeneza mafuta kutokana na karatasi za plastiki

Na FRANKLINE AKHUBULA

YAPATA miaka minne sasa tangu Bw Daniel Ngenga na rafiki yake Patrick Watene walipokutana na kuanzisha urafiki wao.

Kutokana na mazungumzo baina yao ya mnamo 2017, wawili hao ambao hawakuwa na ajira, wakiwa wanafanya vibarua kwa kandarasi, walikubaliana kushirikiana kuanzisha mradi wa kujikimu maishani.

Bw Ndenga alikuwa mkandarasi wa kibinafsi baada kujiuzulu kama mhandisi katika kampuni ya Excide inayouunda betri za gari jijini Nairobi.

Rafikiye Bw Watene kwa upande mwingine alikuwa mshauri wa kikandarasi kwa Shirika la Umeme (Kenya Power and Lighting).

Wanasema kwamba wote walikuwa wanapitia masaibu mengi kimaisha.

Hawangeweza kujikimu maishani kutokana na mapato madogo.

Ni kutokana na sababu hiyo ndipo walipoanza kujadiliana kuhusu njia mbadala za kuboresha maisha na mapato yao.

Bw Ndenga anasema kuwa wakati huo, Kenya ilikuwa imepiga marufuku utumiaji wa mifuko ya plastiki (sandarusi).

Hapo ndipo wazo la kuanzisha kiwanda cha kutengeneza mafuta kutoka kwa plastiki lilipozuka.

“Tuliafikiana kuhusu utengenezaji wa mafuta kutokana na mifuko hiyo iliyoharamishwa kwa sababu lengo letu lilikuwa ni kuchangia katika uboreshaji wa mazingira nchini,” anasema Bw Ndenga.

Dan Ngenga amehitimu elimu ya chuo kikuu na shadada ya Uhandisi wa Kemikali kutoka Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret huku mwenziwe, Bw Patrick Watene akiwa mwanafunzi wa zamani wa Chuo cha Kiufundi cha Kiambu ambako alihitimu kama Mhandisi wa Nguvu-umeme.

Ili kutimiza ndoto yao, wawili hao ambao hawakuwa na fedha za kuanzisha biashara yao, baadaye walianza kutafuta zaidi ya Sh3.5 millioni ambazo wangezitumia kuanzisha mradi wao.

“Haikuwa rahisi kwa sababu hatukuwa na pesa hizo. Baada ya kutafuta mkopo wa fedha hizo kutoka kwa benki kadhaa ili kufadhili mradi wetu japo bila mafanikio, hatimaye tulikopa kila mmoja mmoja kwa mashirika madogo madogo ya mikopo ili kujaliza pengo la akiba yetu tuliyokuwa tumeweka,” asema Ndenga.

Hivyo ndiyo walivyoanzsisha kampuni yao ya Adarsh Polymer yenye makao yake Njiru, jijini Nairobi.

Shughuli za kumimina mafuta kutoka kwa plastiki zimekuwa zikiendelea katika kiwanda chao kwa muda sasa.

Ndenga anasema kuwa kufikia sasa kampuni hiyo imefanikiwa kuajiri takribani wafanyakazi watano wanaotegemea kampuni hiyo moja kwa moja.

Kadhalika, kulingana naye, kampuni hiyo ina uwezo wa kuunda lita 20,000 kwa mwezi ambazo kwa sasa zinauzwa katika kampuni ya East Africa Industries ambayo ndiyo mteja wao mkuu.

Lita moja ya mafuta hayo inagharimu Sh60, ikiwa nafuu ya Sh40 tofauti na Sh100, bei ya mafuta kama hayo kutoka kwa soko la kimataifa.

Kila mwezi, Ndenda na Watene wana uwezo wa kuunda zaidi ya lita 80,000 za mafuta hayo ambayo wanasema hawajapata malalamishi yoyote kutoka kwa wanunuzi.

Mwishoni mwa mwezi, yapata mwaka mmoja tangu kuanza mradi huo, wamekuwa wakipokea pato la Sh1.2 milioni kabla ya matumizi mengine ya kibiashara ikiwemo kulipia umeme na hata kulipa mishahara ya wafanyakazi, miongoni mwa matumizi mengine.

“Tuliegemea kwenye pendekezo la kuunda mafuta kwa sababu licha ya kuleta suluhu kwa tatizo la uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na uwepo wa bidhaa za plastiki na karatasi, ni suluhisho la kudumu kwa shida hii ambayo imekithiri kama janga nchini kwa muda mrefu.

“Vile vile, tulitaka kuchangia katika kuboresha bei ya mafuta nchini kwa kuifanya nafuu zaidi. Kuwepo kwa mafuta ya bei nafuu kutapelekea wanunuzi kupata bidhaa hiyo kwa bei nafuu,” anasema Watene.

Chanzo cha malighafi

Kutokana na juhudi zao, mbali na kupata malighafi kutoka kwa wale ambao wameajiriwa moja kwa moja, huwa wananufaika kutokana na watu wanaookota bidhaa za plastiki na kuuzia kampuni hiyo kabla ya kutumia kama bidhaa za kuunda mafuta hayo.

Hii ni muhimu sana kwani, waokotaji hao wa bidhaa za plastiki huweza kupata riziki yao kutoka kwa kampuni hii.

Kulingana na Ndenga, soko la mafuta ni kubwa sana.

Mbali na kutegea kampunini za humu nchini, wanasema kuwa wanao mpango kabambe wa kuanza kuuza mafuta yao katika mataifa mengine ya bara la Afrika katika muda wa miaka mitano ijayo.

Wanashukuru kampuni ya East African Industries kwa kuwa na imani na mafuta ya kampuni hiyo wakidokeza kuwa ni kutokana na mchango wa kampuni hiyo ndiposa wameweza kuendeleza juhudi zao za kutengeneza mafuta.

Ndenga anatoa ushauri kwa wale ambao wangependa kuanzisha au kufungua kampuni yoyote ile kufanya utafiti kuhusu mradi wowote kabla ya uzinduzi ili kubaini sawasawa mahitaji ya mradi wa sampuli hiyo.

“Tulifanya utafiti wetu kupitia mtandao kando na kuzungumza na wataalamu wengine kabla ya kuelekea Uchina tulikofanya utafiti zaidi na hatimaye kuagiza mashine tunayotumia kutengeneza mafuta haya kiwandani,” anadokezea Bw Ndenga.

Mwaka juzi kampuni ya Adarsh Polymer ilikuwa miongoni mwa kampuni zilizoalikwa kushiriki kwenye kongamano la kimataifa lililofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa UNEP, Gigiri, jijini Nairobi ambako walihusika katika kujadili mbinu mbadala za kupunguza uwepo wa vyombo na makaratais ya plastiki ambayo yametajwa pakubwa kama kizingiti kikuu cha utunzaji mazingira.

Plastiki ni hatari katika uchafuzi wa mazingira kwa kuwa inachukua miaka mingi ili kuoza.

“Tuna mipango pia ya kuanza kutengeneza makaa ya kisasa na kuwafaidi Wakenya kama umeme wa matumizi ya kupikia nyumbani.

“Vilevile, tukipata mashine kubwa, tutaweza kutengeneza lami ambayo itaweza kutumika kuunda barabara zetu hapa Kenya na Afrika nzima,” asema Ndenga.

[email protected]

You can share this post!

Mamia wauawa mpakani mwa Ethiopia na Somalia

TAHARIRI: Huduma za polisi zijumuishe ushauri