• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Gharama ya juu ya matibabu inavyobagua maskini

Gharama ya juu ya matibabu inavyobagua maskini

NA LEONARD ONYANGO

UGONJWA wa corona umejiongeza kwenye orodha ndefu ya maradhi hatari ambayo yamewalazimu Wakenya maskini kutumia mbinu mbadala kuokoa maisha yao baada ya kulemewa na gharama ya juu ya matibabu hospitalini.

Huku vyumba vya kulaza wagonjwa mahututi wa corona katika hospitali za umma vikiwa tayari vimejaa hadi pomoni kote nchini, ni pigo kwa maskini ambao hawamudu gharama ya juu ya matibabu katika hospitali za kibinafsi.

Hospitali za kibinafsi zinahitaji malipo ya awali ya hadi Sh600,000 kabla ya kukubali kulaza mgonjwa wa corona katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Katika Hospitali ya Nairobi, kwa mfano, familia ya mgonjwa wa corona ni sharti ilipe Sh600,000 kwanza kabla ya jamaa yao kukubaliwa kulazwa katika kitanda cha ICU.Katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) familia ni sharti ilipe Sh200,000 kabla ya mgonjwa wa corona kuingizwa kwenye chumba cha ICU.

Familia nyingi zimekuwa zikizunguka kutoka hospitali moja hadi nyingine zikitafuta chumba cha kulaza jamaa wao wanaougua virusi vya corona.Japo vipimo vya corona vinafanywa bila malipo, haswa katika hospitali za kaunti, inagharimu hadi Sh20,000 katika baadhi ya hospitali za kibinafsi.

Katika Hospitali ya Nairobi West, kwa mfano, vipimo vya corona vinagharimu Sh6,000.Familia ya Julius Odhiambo, mnamo Machi, mwaka huu, ilisafirisha baba yao aliyekuwa na matatizo ya kupumua kutoka Kendu Bay, Kaunti ya Homa Bay, hadi jijini Nairobi ikiwa na matumaini kwamba ingepata matibabu ya haraka.

“Tulizunguka katika hospitali mbalimbali jijini Nairobi lakini tuliambiwa kulipa kati ya Sh200,000 na Sh400,000 kwanza kabla ya kulazwa. Sisi tulikuwa na Sh100,000 tu. Tulipiga simu kila mahali tukitafuta usaidizi.

“Hatimaye, nilipigia simu afisa mmoja wa wizara ya Afya, ambaye alitusaidia kupata kitanda katika Hospitali ya Mbagathi baada ya kuhangaika kwa siku tatu,” anasema Bw Odhiambo ambaye ni mwanahabari.

Hata hivyo, baba yake, Mzee James Odhiambo, aliaga dunia chini ya saa 24 baada ya kulazwa.Kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa, wizara ya Afya imekuwa ikitangaza idadi ya juu ya vifo vilivyotokana na corona.

Kulingana na Mkurugenzi wa Matibabu nchini Dkt Patrick Amoth, idadi hiyo inajumuisha vifo vilivyotokea miezi ya nyuma lakini haikujumuishwa kwenye takwimu za wizara ya Afya.

“Kuna vifo vya waathiriwa wa corona vilivyotokea miezi iliyopita katika vituo vya afya au nyumbani ambavyo havikujumuishwa kwenye hesabu ya wizara ya Afya. Kwa sasa tunakagua rekodi za vituo vya afya na kutumia machifu kupata taarifa za vifo vya corona,” anasema Dkt Amoth.

Alhamisi iliyopita, kwa mfano, wizara ya Afya ilitangaza vifo 16 vya corona; idadi hiyo ilijumuisha kifo kimoja kilichotokea ndani ya saa 24, kimoja ndani ya mwezi mmoja na 14 vilivyotokea miezi mingi iliyopita.

Wataalamu wanasema kuwa takwimu hizo za wizara ya Afya ni ithibati kuwa idadi kubwa vya Wakenya wa mapato ya chini wamekuwa wakifariki kutokana na corona nyumbani kwa kushindwa kumudu gharama ya juu matibabu.

Wakili Donald Kipkorir hivi karibuni alielezea kuwa ametumia Sh4 milioni kupata huduma za matibabu alipoambukizwa na virusi vya corona.Wakili huyo aliezea namna alivyowekewa mitambo ya kumsaidia kupumua baada ya mapafu kulemewa.

Bw Emmanuel Atamba, wiki iliyopita, alitumia mtandao wa kijamii kuelezea jinsi mkewe alianza kujitibu kwa kutumia tembe za ‘azithromycin’ na kula matunda ya akila aina ‘kuimarisha’ kingamwili baada ya kupatikana na virusi vya corona.

Baada ya siku 10, dalili za ugonjwa wa corona zilitoweka lakini mkewe aliendelea kuwa dhaifu. Baada ya siku chache alikuwa na tatizo la kupumua.

“Mke wangu alipozidiwa nilimpeleka hospitalini na akalazwa ICU. Muuguzi alinieleza kuwa mke wangu alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kumeza tembe za azithromycin,” akaelezea.

Tembe za azithromycin hutumika kutibu maradhi yanayosababishwa na bakteria kama vile nimonia.Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), tembe za kutibu maradhi yanayosababishwa na bakteria haziwezi kutibu magonjwa yanayosababishwa na virusi. Corona ni ugonjwa unaosababishwa na virusi.

Shirika la WHO linashauri kuwa dawa za bakteria (antibiotics) zinafaa kutumiwa tu baada ya kupewa ushauri na daktari.Idadi kubwa ya Wakenya maskini sasa wanatumia dawa za bakteria na matibabu ya kiasili kama vile kujifukiza, kunywa mchanganyiko wa ndimu, tangawizi na kitunguu saumu kati ya njia nyinginezo kujitibu virusi vya corona.

Ugonwja wa corona sasa umejiunga na maradhi mengine hatari kama vile, kansa, kisukari, moyo, shinikizo la damu, Hepatitis C, nakadhalika, ambayo ni ghali kutibu.

Kansa

Utafiti uliofanywa 2018 katika vituo mbalimbali vya kutibu kansa jijini Nairobi, ikiwemo Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), Hospitali ya Nairobi na Hospitali ya Aga Khan, ulionyesha kuwa idadi kubwa ya Wakenya hawawezi kumudu matibabu ya saratani.Inagharimu kati ya Sh172,000 na Sh759,000 kutibu kansa ya mlango wa uzazi (cervical cancer), bila kufanyiwa upasuaji.

Inagharimu kati ya Sh672,000 na Sh1.25 milioni kwa mwathiriwa wa kansa ya mlango wa uzazi kufanyiwa upasuaji, kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa na Taasisi ya Kansa nchini (NCIK) na Idara ya Kudhibiti Kansa nchini (NCCPK).

Matibabu ya kawaida ya kansa ya matiti yanagharimu kati ya Sh175,200 na Sh1.98 milioni na gharama huongezeka hadi Sh2.48 milioni kufanyiwa upasuaji.

Kansa ya korodani (prostate) inagharimu kati ya Sh138,000 na Sh1.21 milioni huku kansa ya koo ikigharimu zaidi ya Sh1 milioni.Kupima kansa ya matiti ni inakagharimu Sh15,000, kwa mujibu wa wa ripoti hiyo.

Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa Wakenya 47,000 hupatikana na kansa huku wengine 32,000 wakifariki kila mwaka.Inakadiriwa kuwa wanawake 5,900 hupatikana na kansa ya matiti kila mwaka. Asilimia 43 ya wanawake humu nchini wameshindwa kupata matibabu kutokana na gharama ya juu ya matibabu ya kansa.

Baadhi ya Wakenya wanaojimudu husafiri hadi katika mataifa ya kigeni kutafuta matibabu ya magonjwa sugu kama vile kansa.Kati ya Januari na 2019, wagonjwa 400 waliruhusiwa na wizara ya Afya na Baraza la Madaktari na Wataalamu wa Meno (KPDC) kwenda kutibiwa katika mataifa ya kigeni kama vile Afrika Kusini, Ujerumani, India na Uingereza, kulingana na mkurugenzi wa KPDC, Dkt Daniel Yumbya.

Kusafiri nje ya nchi huwa ghali kwani mgonjwa analazimika kulipia gharama ya matibabu, malazi hotelini au ndani ya hospitali, tiketi ya ndege na chakula.

Mara nyingi mgonjwa husafiri na mwangalizi ambaye anafanya gharama kwenda juu.Tafiti mbalimbali ambazo zimefanywa zimebaini kuwa inagharimu angalau Sh60,000 kutibu wagonjwa wa kisukari kwa mwaka. Wagonjwa wa kisukari huhitaji dawa ya kuteremsha kiwango cha sukari mwilini ambayo hutumia maisha yao yote.

Ni vigumu kwa watu wa mapato ya chini kupata kiasi hicho cha fedha kupata matibabu ya kisukari.Utafiti uliofanywa 2017 na wizara ya Afya kuhusu gharama ya maradhi ya kifua kikuu (TB) ulibaini asilimia 50 ya Wakenya hawapimwi au kutibiwa.

Kulingana na ripoti ya utafiti huo, familia zilizo na mgonjwa wa TB hutumia wastani wa Sh26,000 kutafuta matibabu kwa mwaka.Asilimia 27 ya waathiriwa wa TB hulazimika kuchukua mikopo au kuuza mali zao ili kutafuta matibabu.

You can share this post!

CECIL ODONGO: Muungano wa Raila, Ruto utamtakasa Naibu wa...

Mwalimu Mkuu alivyojitoa mhanga kufanikisha elimu