• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
BENSON MATHEKA: Serikali itimize onyo la wataalamu kuhusu mvua

BENSON MATHEKA: Serikali itimize onyo la wataalamu kuhusu mvua

Na BENSON MATHEKA

KWA sasa mvua inanyesha katika baadhi ya maeneo nchini. Idara ya utabiri wa hali ya hewa imeonya kuwa mvua ya masika mwaka huu huenda ikawa chache na baadhi ya maeneo ya nchi hayatapata mvua kamwe.

Hili ni onyo la wataalamu na halifai kupuuzwa baadhi ya watu wakiwemo maafisa wa serikali wanavyofanya.

Wataalamu hao wameshauri wakulima wanaotegemea mvua, kupanda mimea inayostahimili kiangazi kama mihogo, viazi vitamu na mtama.

Hivi ndivyo, watafiti wa kilimo wamekuwa wakiambia wakulima.

Huu ni ushauri unaofaa ambao unabaki kuwa ripoti za utafiti kwa sababu wakulima hawasaidiwi kuutekeleza.

Haifai kwa maafisa wa serikali kutumia pesa za umma kuzuru maeneo tofauti kuwahimiza wakulima wa mashamba madogo kutumia mbinu za kisasa na kukumbatia kilimo cha mimea inayostahimili ukame kisha watarajie wafanye hivyo bila kuwasaidia kwa mbegu na pembejeo zinazohitajika.

Kuambia mkulima ambaye hana uwezo wa kununua chakula cha siku anunue mbegu za kisasa ni sawa na kumtaka mlemavu wa mguu atembee.

Hii ni kinaya kwa serikali ambayo imeorodhesha utoshelevu wa chakula na lishe kama moja ya ajenda zake kuu.

Wataalamu wamefanya kazi yao licha ya changamoto za kifedha zinazowakabili.

Wale wa hali ya hewa wametoa ushauri wao na wale wa Shirika la Utafiti wa Kilimo na Ufugaji (KALRO) wamefanya kazi ipasavyo.

Hata hivyo, wale wanaofaa kutekeleza ripoti zao, wakiwemo viongozi wa kisiasa hawana nia njema ya kumaliza tatizo la uhaba wa chakula nchini.

Wangekuwa na nia njema, wangekuwa wametenga pesa za kusambazia wakulima mbegu zinazofaa maeneo yao, mbolea na dawa.

Wangekuwa wanaweka sera ya kilimo ya kuwamotisha wakulima badala ya kuwavunja moyo.

Tunachoshuhudia na kusikia kutoka kwa viongozi na wanasiasa ni maneno matamu tu kuhusu mipango ya kuhakikisha nchi ina chakula cha kutosha.

Kila wakati maeneo kadhaa yanapokubwa na ukame, kauli ya viongozi hao huwa ni moja; kwamba hakuna Mkenya atakayekufaa njaa kwa kuwa serikali imeweka mikakati ya kutosha.

Wanaposema haya wakiwa katika maofisi yao ya kifahari ya serikali kuu au serikali za kaunti, Wakenya masikini maeneo ya mbali mashambani huwa wamezika wenzao wanaofariki kwa njaa.

Maelfu ya mifugo huwa inaendelea kuangamia kwa sababu ya ukame ambao, wataalamu wa serikali yenyewe huwa wameonya utatokea na kuishauri serikali kuchukua hatua za kuzuia hasara.

Hali hii itaendelea kujirudia nchini iwapo ushauri wa wataalamu utaendelea kupuuzwa.

You can share this post!

MAUYA OMAUYA: Amri ya kafyu imegeuka soko la rushwa

JAMVI: Karata za Uhuru zinavyohatarisha Mlima Kenya...