• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
ODONGO: Kwa kumpinga Raila, Obado anajiua kisiasa

ODONGO: Kwa kumpinga Raila, Obado anajiua kisiasa

Na CECIL ODONGO

GAVANA wa Migori Okoth Obado anaendelea kijichimbia kaburi la kisiasa baada ya kujitokeza kumpinga kinara wa ODM Raila Odinga na ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI).

Baada ya kugundua kuwa muhula wake wa pili unakamilika, gavana huyo ambaye amekuwa na uhusiano vuguvugu na Bw Odinga sasa anaonekana kuchoshwa na uongozi wa ODM huku akikumbatia chama cha PDP kinachoongozwa na mwanasiasa wa Tangatanga Omingo Magara.

Ingawa ana haki ya kugombea wadhifa wowote ule unaofaa baada ya kutamatisha muhula wake wa pili kama Gavana, Bw Obado anafaa ajihadhari katika safari yake mpya ya kisiasa ili asifuate mkondo wa baadhi ya wanasiasa waliompinga Bw Odinga zamani na wakajipata wamejitumbukiza katika kaburi la sahau kisiasa.

Baada ya mfumo wa vyama vingi kukumbatiwa 1992, kila anayeazimia kutwaa wadhifa wowote wa kisiasa yu huru kufanya hivyo, ila ukweli ni kwamba siasa za Kenya bado zina miegemeo ya kikabila na ushawishi wa viongozi wakuu wa kieneo.

Iwapo Bw Obado alifahamu kuwa bado alikuwa na umaarufu kwa nini alikigura PDP alichotumia kushinda ugavana pembamba 2013 na kurejea ODM kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017.

Bila shaka aligundua kwamba mawimbi makali ya chama hicho Migori yangemsomba ndiposa akaamua kupigania tiketi na kumbwaga seneta wa sasa Ochilo Ayacko wakati wa uteuzi wa ODM.

Hata hivyo, inaonekana gavana huyo alihitaji tu ODM kuingia mamlakani kipindi chake cha pili cha uongozi kisha ageuke ghafla na kuanza maasi akilenga kiti kingine. Hii ni tabia ambayo imekuwa ikitumiwa na viongozi ambao wana uchu wa uongozi na gavana huyo si wa kwanza.

Wakati wa uchaguzi mdogo wa useneta Migori mnamo Oktoba 2018, Bw Obado alikaidi ODM na kuanza kupima umaarufu wake kisha kumuunga mkono mwaniaji wa chama cha FPK Eddy Oketch Gicheru aliyeshindwa na Bw Ayacko.

Aidha kabla ya kupitishwa kwa ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) Migori ilidaiwa kuwa Bw Obado alikuwa na uvuguvugu huku akiipinga kichichini. Baadhi pia wamekuwa wakidai kwamba ni Bw Odinga ndiye aliwashawishi madiwani wasipige kura ya kumwondoa mamlakani mnamo Septemba mwaka jana.

Japo kauli aliyoitoa kuwa BBI huenda isiwanufaishe raia jinsi inavyodaiwa, kauli ya madiwani wa ODM Migori kuwa anafaa atimuliwe chamani au ajiondoe ugavana inaafiki.

Inashangaza kuwa ODM ilikuwa chama kinachozingatia demkorasia wakati alipohitaji ugavana lakini chama dhalimu baada ya kuafikia malengo yake.

Bw Obado ikiwa anajiona mhimili wa siasa za Migori na Nyanza, anafaa ajiuzulu na kusaka ugavana upya jinsi alivyofanya Bw Odinga 1995 alipokosana na kinara wa Ford Kenya wakati huo marehemu Kijana Wamalwa.

Kuna wanasiasa waliokuwa na umaarufu na waliojaribu kumponya Bw Odinga ufalme wa siasa za Nyanza lakini mwishowe wakazama wasisikike tena huku baadhi wakinywea na kumtii.

Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju, seneta wa Siaya James Orengo, mtaalamu wa teknolojia Shem Ochuodho, aliyekuwa mbunge wa Karachuonyo James Rege miongoni mwa wengine waliwahi kufuata njia anayojaribu Bw Obado na kufeli kabisa.

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali izingatie ripoti za watafiti

WANGARI: Uteuzi wa jaji mkuu mpya utekelezwe kwa makini