• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Zamu ya Fred Ngatia mbele ya jopo la JSC kwenye mchakato wa uteuzi wa Jaji Mkuu

Zamu ya Fred Ngatia mbele ya jopo la JSC kwenye mchakato wa uteuzi wa Jaji Mkuu

Na SAMMY WAWERU

WAKILI Fred Ngatia ametetea vikali kauli yake ya kutokuwa na akaunti yoyote ya mitandao ya kijamii kipindi hiki ambapo idara ya mahakama inajikakamua kukumbatia mfumo wa teknolojia ya kisasa kuimarisha utendakazi.

Mapema Jumanne, wakili huyo mwenye tajriba ya takribani muda wa miaka 41 katika masuala ya uanasheria wakati akihojiwa na jopo la tume ya kuajiri watumishi katika idara ya mahakama (JSC) kuwania wadhifa wa Jaji Mkuu (CJ), alisema hana akaunti yoyote ya mitandao ya kijamii.

Bw Ngatia alisema ni uamuzi wa kibinafsi, kuyafanya maisha yake kuwa ya faragha.

Hata hivyo alipotakiwa kueleza jinsi atakavyoweza kufanikisha uimarishaji wa huduma za mahakama kupitia mifumo ya teknolojia ya kisasa, alisema hapingi mkondo huo.

“Idara ya Mahakama Uingereza ina tovuti inayofanya kazi bora; jukwaa ambalo unaweza kufuatilia kila hatua ya jaji na mawasilisho ya mawakili,” Bw Ngatia akasema, akieleza kwamba endapo atateuliwa kuwa Jaji Mkuu ataiga nyayo za Uingereza.

Wakili huyo alisema amekwepa kuwa mitandaoni kwa sababu ya visa vya watu kushambuliwa wangachiaji mitandao.

Kiti cha Jaji Mkuu kilisalia wazi kufuatia kustaafu kwa CJ David Maraga mwishoni mwa 2020.

Kesi ya kupinga matokeo ya kura za urais

Amesema kesi ya kupinga  kuchaguliwa kwa Rais na naibu wake inastahili kusikilizwa na mahakama ya juu zaidi.

Bw Ngatia amesema hayo Jumanne mbele ya makamishna wa kamati ya tume ya huduma za mahakama (JSC), inayoendeleza zoezi la kuwahoji wanaowania wadhifa wa Jaji Mkuu (CJ).

Kiti hicho kilisalia wazi kufuatia kustaafu kwa CJ David Maraga, mwishoni mwa mwaka uliopita, 2020 baada ya kukamilisha kipindi chake cha muda wa miaka 4.

“Wakili Ngatia, ningependa ueleze makamishna kesi ya kupinga kuchaguliwa kwa rais pingamizi inapoibuka inapaswa kusikilizwa na korti ipi?” akauliza Naibu Jaji Mkuu, Bi Philomena Mwilu na ambaye ni kaimu Jaji Mkuu.

Bw Ngatia alijibu, inapaswa kusikilizwa na mahakama ya juu zaidi, akisema kesi ya aina hiyo ikiwasilishwa kwa korti za chini rufaa nyingi zitachipuka.

“Mahakama ya juu zaidi ndiyo inapaswa kusikiliza kesi ya aina hiyo. Ikiwasilishwa kwa korti za chini rufaa nyingi zitaibuka,” wakili Ngatia akasema.

Bw Ngatia ni kati ya wanaomezea mate kiti cha CJ, na Jumanne ilikuwa zamu yake kuhojiwa na kupigwa msasa.

Kufuatia uchaguzi tata wa 2017, wakili huyo alikuwa miongoni mwa waliomwakilisha Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake Dkt William Ruto, baada ya kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga chini ya muungano wa Nasa kupinga katika mahakama ya juu zaidi kuchaguliwa kwa wawili hao.

Mahakama hiyo ilifutilia mbali ushindi wao, baada ya kikosi cha Bw Odinga kuishawishi kupitia ushahidi wa kutosha uchaguzi ulisheheni udanganyifu.

Mahakama hiyo iliamuru Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuandaa marudio ya uchaguzi wa kiti cha urais. Bw Odinga hata hivyo hakushiriki.

Kwa sasa kiongozi huyo wa upinzani anashirikiano kwa karibu na Rais Kenyatta, baada ya wawili hao kutangaza Machi 2018 kuzika tofauti zao za kisiasa kupitia salamu za maridhiano maarufu kama Handisheki.

You can share this post!

Mwanatenisi Okutoyi atupwa chini nafasi sita, anashikilia...

Wadau waidhinisha mpango wa kupanua ushiriki wa UEFA kutoka...