• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Mwanatenisi Okutoyi atupwa chini nafasi sita, anashikilia nambari 161 duniani sasa

Mwanatenisi Okutoyi atupwa chini nafasi sita, anashikilia nambari 161 duniani sasa

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Angella Okutoyi ameteremka nafasi sita kwenye viwango bora vya Shirikisho la Kimataifa la Tenisi (ITF) vya chipukizi ambavyo vilitolewa Aprili 19.

Mchezaji huyo wa tenisi, ambaye sasa anashikilia nafasi ya 161 duniani, alishuka kwenye viwango hivyo kutokana na kuondolewa mapema katika mashindano ya daraja ya tatu ya J3 Megrine.

Okutoyi,17, alilemewa na Liisa Varul (Estonia) kwa seti 2-1 za 6-0, 4-6, 6-2 katika raundi ya pili mjini Megrine, Tunisia.

Akiorodheshwa wa kwanza kabla ya mashindano, Okutoyi alianza kampeni yake mjini Megrine kwa kubwaga Mmoroko Manal Ennaciri japo kwa jasho 6-4, 7-6 mnamo Aprili 13 kabla ya kubanduliwa na Varul.

Okutoyi alishirikiana na Celine Siminyu kutoka Ireland katika mchezo wa wachezaji wawili kila upande. Walilima timu ya Ennaciri na Ubelgiji Romane Longueville 6-2, 6-3 katika raundi ya kwanza kabla ya kuzimwa na Waitaliano Carlotta Moccia na Emma Valleta 4-0, 2-4, 10-2 katika raundi ya pili.

Okutoyi aliingia shindano la Megrine akiorodheshwa nambari 155 duniani, nao Ennaciri na Varul walikamata nafasi ya 559 na 496, mtawalia. Varul amepaa nafasi 39 na kutulia katika nafasi ya 457 baada ya kufika nusu-fainali naye Ennaciri amerushwa chini nafasi tatu.

“Mchezo wake mjini Megrine hauwezi kutiliwa shaka kutokana na usumbufu huu wote uliosababishwa na janga la virusi vya corona,” alisema Francis Rogoi alipoulizwa kuhusu matokeo ya Okutoyi. Rogoi alikuwa kocha wa Okutoyi alipozoa mataji mawili ya daraja ya nne jijini Nairobi mwezi Januari.

Okutoyi alipaa nafasi 59 na kukalia nafasi ya 127 duniani baada ya mafanikio ya Nairobi. Alielekea katika kituo cha kukuza talanta cha Casablanca nchini Morocco mwezi Februari. Katika shindano lake la kwanza tangu Januari, Okutoyi aliduwazwa na kinda wa miaka 13 kutoka Morocco Amina Zeghlouli kwa seti mbili bila jibu katika raundi ya kwanza ya J5 Sfax mnamo Aprili 6.

You can share this post!

Omala ajiandaa kwenda Uswidi kusakatia Linkoping City

Zamu ya Fred Ngatia mbele ya jopo la JSC kwenye mchakato wa...