• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 10:50 AM
TAHARIRI: Pendekezo la EPRA lina umuhimu gani?

TAHARIRI: Pendekezo la EPRA lina umuhimu gani?

KITENGO CHA UHARIRI

WIKI jana Tume ya Kudhibiti Kawi (EPRA) iliamua kuendelea na bei ya mafuta iliyokuwa imetumika kwa mwezi mmoja, bila ya kuifanyia mabadiliko.

Uamuzi huo wa kushangaza, huenda ulitokana na taarifa zilizokuwa zimechapishwa kwenye vyombo vya habari. Taarifa hizo zilionyesha tume hiyo ilipanga kupandisha bei ya mafuta ya petroli kwa angalau Sh7 kwa lita.

Baadaye, EPRA ilitoa taarifa kuonyesha hakutakuwa na mabadiliko ya bei. Lakini ni wazi hatua hiyo ilichukuliwa kuonyesha kuwa vyombo vya habari havikuwa sahihi, na kwamba taarifa iliyochapishwa ilikuwa feki.

Hata hivyo, baada ya hapo serikali haikufurahishwa na hatua ya vyombo vya habari. Sasa kupitia waziri wa Madini na Petroli, serikali inapendekeza sheria itakayoharamisha wanahabari kuchapisha habari kabla hazijatolewa rasmi.

Sheria hiyo inapendekeza kuwa mtu atakayepatikana na hatia ya kuvunja sheria hiyo, atatozwa faini isiyopungua Sh100,000.

Hatua hii ya serikali na EPRA ni uhatari kwa taaluma ya kanuni za uanahabari. Sekta hiyo inakua kila siku na haitarajiwi kuendeshwa kama ilivyokuwa miaka kumi iliyopita. Badala ya wanahabari kuketi na kusubiri wapewe taarifa, ulimwengu sasa hivi unawatarajia wachanganue na hata kufananisha kwa mfano bei ya mafuta ya miezi iliyotangulia. Kisha katika upambanuzi huo, wataalamu wa masuala ya uchumi au wa sekta ya mafuta wanaweza kutoa ubashiri wao.

Hata kama kweli wanahabari walikuwa na fununu kuhusu bei iliyokuwa itangazwe, kuna ubaya gani kusema hivyo?

Ripoti ya kupanda au kupungua kwa bei ya mafuta si siri ya serikali inayoweza kuhatarisha usalama wa nchi. Wenye magari ya uchukuzi wa umma na watumiaji wengine wa mafuta wamekuwa wakilalama tu na hatimaye kuongeza nauli kidogo. Kuwatahadharisha na mapema kwamba bei itapanda ni njia ya kuwaonya wajipange wakati huu ambapo hali ya uchumi ni ngumu.

Lengo la uanahabari ni kuwakilisha maslahi ya umma. Iwapo kwa kudokeza mapema kuwa bei ya mafuta inatarajiwa kupanda au kushuka, umma utakuwa na habari ya kuuwezesha kuangalia upya najeti yake, kwa nini iwe ni hatia?

You can share this post!

Rais wa Chad afariki vitani baada ya kuchaguliwa tena

WASONGA: Uteuzi wa makamishna wapya wa IEBC uwe na uwazi