• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Rais wa Chad afariki vitani baada ya kuchaguliwa tena

Rais wa Chad afariki vitani baada ya kuchaguliwa tena

Na MASHIRIKA

N’DJAMENA, Chad

RAIS wa Chad aliyechaguliwa upya Idriss Deby alifariki akiwa na umri wa miaka 68 kutokana na majeraha aliyopata vitani.

Deby alikuwa amekwenda kuzuru wanajeshi wanaopigana na waasi katika eneo la Sahel, Kaskazini mwa nchi hiyo, msemaji wa jeshi alisema Jumanne.

“Derby alivuta pumzi ya mwisho akilinda taifa tukufu kwenye uwanja wa vita wikendi,” msemaji wa jeshi Jenerali Azem Bermandoa Agouna, alisema kupitia taarifa iliyosomwa katika runinga ya kitaifa.

Jenerali Mahamat Kaka, mwanawe marehemu kiongozi huyo wa Chad, alitangazwa kama kaimu rais wa taifa hilo kulingana na Agouna.

Ripoti hizo zilijiri siku moja tu baada ya Deby, aliyechukua mamlaka mnamo 1990 kupitia uasi, kushinda hatamu ya sita kulingana na matokeo ya awali yaliyotangazwa Jumatatu.

Alinyakua asilimia 79.3 ya kura katika uchaguzi wa urais uliofanyika Aprili 11, kulingana na matokeo hayo.

Deby aliahirisha hotuba yake ya ushindi kwa wafuasi wake na badala yake akaenda kuzuru wanajeshi wa Chad wanaokabiliana na vikosi, alisema meneja wa kampeni yake.

Kundi la waasi kwa jina Front for Change and Concord in Chad (FACT), lenye makao yake kwenye ukanda wa Kaskazini nchini Libya, walipata pigo wikendi wakati vikosi vya jeshi vilipowaua wapiganaji zaidi ya 300 na kuwachukua mateka 150 Jumamosi, katika mkoa wa Kanem karibu kilomita 300 (maili 185) kutoka jiji kuu la N’Djamena.

Wanajeshi watano wa serikali waliuawa huku 36 wakijeruhiwa, kulingana na Agouna.

Deby alikuwa mwana wa mfugaji kutoka kabila la Zaghawa, aliinuka mamlakani kupitia jeshi na alienzi utamaduni wa kijeshi.

Ushindi wake mpya katika uchaguzi haukuwahi kutiliwa shaka huku kukiwa na upinzani uliogawanyika, wito wa kususia kura na kampeni ambapo maandamano yalipigwa marufuku au kutawanywa.

Deby alikuwa amefanya kampeni kwa ahadi ya kuleta amani na usalama eneo hilo lakini ahadi zake zilihujumiwa na uvamizi wa waasi.

Taharuki ilizuka Jumatatu katika baadhi ya maeneo ya N’Djamena baada ya matangi kuwekwa katika barabara kuu za jiji, ripoti zilisema.

Matangi hayo yaliondolewa baadaye isipokuwa kwenye eneo linalozingira afisi ya rais, ambayo hulindwa vikali i nyakati za kawaida.

Ubalozi wa Amerika jijini N’Djamena Jumamosi uliwaamrisha maafisa wasiotoa huduma muhimu kuondoka nchini humo, wakionya kuhusu uwezekano wa kuzuka kwa ghasia.

Uingereza pia iliwatahadharisha raia wake kuondoka.

You can share this post!

NASAHA ZA RAMADHAN: Aliyefunga azingatie zaidi Ucha Mungu...

TAHARIRI: Pendekezo la EPRA lina umuhimu gani?