• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Korti yamzima Orengo kuwa wakili wa Manduku

Korti yamzima Orengo kuwa wakili wa Manduku

Na PHILIP MUYANGA

MAHAKAMA Kuu imemzima Seneta wa Siaya, James Orengo, kumtetea aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari ya Kenya (KPA) Dkt Daniel Manduku.

Jaji Eric Ogola aliamua kwamba akiwa seneta, Bw Orengo ni afisa wa serikali na hafai kumwakilisha Dkt Manduku.Uamuzi huo unaweza kuwafungia nje wabunge wengine mawakili kuwakilisha maafisa wa serikali wanaoshtakiwa kwa makosa ya ufisadi.

Uamuzi huo ulifuatia kesi ambayo iliwasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kutaka Bw Orengo au maafisa wengine wa serikali kumwakilisha Dkt Manduku katika kesi yake.

Katika kesi hiyo, Dkt Manduku anataka DPP azuiwe kumfungulia mashtaka yoyote kuhusiana na ripoti ya uchunguzi na mapendekezo ya Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI).

Jaji Ogola alisema iwapo Dkt Manduku ataitwa kufika mbele ya Seneti, Bw Orengo atakuwepo kama seneta na hata kama atajiondoa, itakuwa imechukuliwa anaweza kumpendelea.

“Mlalamishi yuko huru kutafuta wakili mwingine wa kumwakilisha lakini sio Orengo,” Jaji Ogola alisema.“Dkt Manduku hana haki ya kuwakilishwa na mtu anayeweza kumuita Bungeni,” alisema Jaji Ogola.

Kwenye kesi yake, DPP ilitaka mahakama kuamua kwamba hatua ya Bw Orengo au afisa mwingine wa serikali kuendelea kuwakilisha Bw Manduku ni kinyume cha Sura ya Sita ya katiba.

Naibu msaidizi mkuu wa DPP, Alexander Muteti pia alitaka mahakama iagize Dkt Manduku kumwajiri wakili ambaye sio afisa wa serikali kumwakilisha.

Bw Muteti alisema kwamba Bw Orengo ni seneta wa Kaunti ya Siaya na kwa hivyo ni afisa wa serikali ambaye sheria inasema hafai kushiriki kazi nyingine ya mshahara.

Bw Muteti alisema kwamba Dkt Mutuku ambaye alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika linalofadhiliwa na mlipa ushuru, aliwajibika kwa umma kupitia kamati za bunge zinazochunguza matumizi ya pesa za umma.

You can share this post!

Madaktari walioenda Cuba warejea Kenya kuanza kazi

LEONARD ONYANGO: Magavana waliofuja fedha za corona...