• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
AKILIMALI: Mbinu safi ya kuzalisha mbegu za viazi vya Kizungu visivyoathiriwa na maradhi

AKILIMALI: Mbinu safi ya kuzalisha mbegu za viazi vya Kizungu visivyoathiriwa na maradhi

Na PETER CHANGTOEK

VIAZI ni miongoni mwa vyakula vinavyotegemewa mno nchini Kenya. Maadamu viazi ni chakula cha pili kinacholiwa kwa wingi na Wakenya, baada ya mahindi.

Hivyo, ipo haja ya kuwepo kwa mbegu bora za kuleta mazao mengi katika muda mfupi. Lakini hali halisi sokoni ni kwamba mazao ni machache ikilinganishwa na hitaji kubwa la wateja.

Mojawapo ya sababu za kuwepo kwa hali hii ni mbegu duni ambazo hazioti wala kukomaa ipasavyo. Wakulima wengi wanalazimika kurudia kupanda mbegu zile zile, na matokeo yake ni mavuno duni.Kwa mujibu wa Baraza la Kitaifa la Viazi Kenya (NPCK), kiwango cha mbegu za viazi kinachohitajika nchini kila mwaka ni tani laki moja.

Lakini ni tani 5,000 pekee ambazo huzalishwa.Ni kwa sababu hii ambapo wataalamu wamebuni teknolojia mpya ya kuzalisha mbegu za viazi vinavyokua kwa haraka na wingi ili kuziba pengo hilo.

Mbinu hii mbadala haihitaji kutumia mchanga.Katika shamba la Tumaini Farm, Kaunti ya Nyandarua, teknolojia hii mpya inayofahamika kwa kimombo kama aeroponics ndiyo inatumika.

Shamba hilo ndilo la pili lenye kutumia mbinu hiyo ya kisasa ya kuzalisha mbegu za viazi eneo zima la Afrika Mashariki. Hapa mbegu huzalishwa kwa kuning’inia hewani au kwenye mazingira yaliyo na unyevunyevu, pahali palipojengwa.

Kwa mujibu wa mtaalamu anayesimamia shughuli hiyo, Ken Nyakang’o, wanatumia mbinu hiyo sababu huzalisha mbegu za viazi kwa wingi. Lengo lao, aeleza, ni kuchangia katika kuafikia maono ya taifa ya kuwa na chakula cha kutosha nchini. Isitoshe, teknolojia hiyo hutumia gharama ya chini.

Mbegu huzalishwa katika maboksi spesheli ndani ya vivungulio huku halijoto ikidhibitiwa. Hivyo, wadudu hawawezi kuingia humo wala mbegu kuathiriwa na magonjwa kwa urahisi.Pia zinasifiwa kwa kusaidia kutunza mazingira kwani yanahifadhi maji na kupunguza nguvukazi.

“Tunazalisha aina mbili za viazi; Shangi na Dutch Robjin,” aeleza Nyakong’o.Mbegu hizo hutolewa katika mashirika ya serikali ya kilimo – Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo (KALRO) na Taasi ya Ukaguzi wa Afya ya Mimea (KEPHIS).

Maboksi hayo maalumu hufungwa kwa karatasi za sandarusi aina mbili; zenye rangi nyeupe na zenye rangi nyeusi, ili kuwezesha mimea kuota mizizi.

Aneleza Nyakong’o: “Karatasi nyeusi ni za kuzuia kumulikwa na mwangaza ili zisinyauke. Zile nyeupe husaidia katika mchakato wa kutengeneza lishe ya mimea.”

Viazi hivyo huning’inizwa hewani na hunyunyiziwa maji yaliyochanganywa na virutubisho. Pia, hunyunyiziwa dawa za kuzuia ugonjwa wa mabaka.Ndani ya vivungulio, mbegu hizo hupitishwa kwa hatua nyingine tatu kabla kuwa tayari kuuziwa wakulima.

“Wiki mbili baada ya mimea kutolewa kwa trei maalum, hunyunyiziwa maji. Kisha baada ya wiki ya tatu, virutubisho vya ziada hunyunyizwa,” aongeza mtaalamu huyo.

Shambani, mbegu hizi huanza kutoa viazi baada ya siku 30 hadi 45 tangu upanzi.Mazao huwa tayari kuvunwa baada ya miezi miwili na nusu. Kila mmea huzaa viazi 60 hadi 70 kwa msimu.

Nyakong’o anasema kuwa tayari wanasambaza mbegu ambazo wamezalisha katika shamba hilo.Wakulima wakishapata mavuno yao huuza kiazi kimoja kwa Sh15 huku gunia la kilo 50 likiuzwa kwa Sh5,000.

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Twataka majibu kuhusu...

AKILIMALI: Amegeuza taka ya mifupa, mayai kuwa mbolea asili