• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
NASAHA: Ni muhimu kwa muumini kudumu katika kuomba msamaha

NASAHA: Ni muhimu kwa muumini kudumu katika kuomba msamaha

Na KHAMIS MOHAMED

TUMO ukingoni mwa kumi la kusamehewa. Katika mwezi huu wa toba, Waislamu wamepata fursa nyingine tena ya kunufaika na Msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa hivyo ndugu wafungaji tulio na nyoyo zilizojaa dhambi, njooni tupae mbinguni kwa pamoja kwa kutumia mabawa ya toba ili tupate kunufaika na rehema, msamaha na maghfira ya Mwenyezi Mungu.

Inavyojulikana hakuna alie salimika na dhambi, kwa sababu hii mwanadamu anayo haja sana ya kutubia asubuhi na jioni, kila wakati haswa katika msimu huu wa Ramadhani.

Daima Mwenyezi Mungu amefungua na kuiweka wazi milango yote ya toba. Mwenyezi Mungu humsamehe mwanadamu yeyote anayejirudi na kuomba msamaha wa kweli.

Hata katika mojawapo ya aya za Quran tukufu tunaambiwa tusikate tamaa katika kufanya toba na kuomba msamaha kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye anayesamehe na mwenye huruma.Quran tukufu pia imebainisha kwamba waumini wenye kuomba toba watapata faraja mbele ya Mwenyezi Mungu.

Vile vile tunaambiwa kwamba tunapojiepusha na dhambi kubwa, basi Mwenyezi Mungu hutufunikia dhambi ndogo na kutufariji katika sehemu bora.Muumini wa Kiislamu anajukumu la kuomba toba na msamaha kwa Mwenyezi Mungu.Wasomi wa Kiislamu wanasema kwamba toba ni jukumu linaloendelea kuanzia mwanzo hadi mwisho wa maisha ya mwanadamu.

Mwanadamu hahitaji njia au mtu ili afanye toba bali hutakiwa kumuomba Mwenyezi Mungu moja kwa moja. Wanadamu wanapaswa kuomba toba maishani.

Mtume Muhammad (SAW) naye katueleza faida ya kufanya Istighfaar kama ilivyo simuliwa na Hadhrat Abbaas (RA) kwamba Mtume (SAW) alisema, “Yule mtu anayeshikamana na Istighfaar, Mwenyezi Mungu humtengenezea njia ya kutoka kwenye kila dhiki. Humtengenezea njia ya faraja kutoka kwenye kila shida na humpatia riziki katika njia zile ambazo hata hawezi kuzidhania.”

Twakuomba ewe msamehevu! Uturuzuku toba ya kikweli kweli, twajivua kabisa kutoka kwenye dhambi na kuyaacha kabisa.Twajuta kwa yale tuliyoyatenda ya makosa na madhambi.

Twaazimia kutoyarudia tena. na kushikamana na twaa yako twaomba utusamehe ewe Msamehevu.Ewe Mwenyezi Mungu, hakika wewe ni Msamehevu unapenda kusamehe, basi twaomba utusamehe, ewe Allah ulitwambia wewe ni msamehevu.

You can share this post!

Uingereza wapewa Ireland ya Kaskazini kwenye mchujo wa...

Wakili kortini kwa madai ya kulaghai mayatima Sh100m