• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
Aston Villa wadidimiza matumaini ya Everton kushiriki soka ya UEFA muhula ujao

Aston Villa wadidimiza matumaini ya Everton kushiriki soka ya UEFA muhula ujao

Na MASHIRIKA

KOCHA wa Everton, Carlo Ancelotti amekiri kwamba matumaini yao ya kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao yamedidimia kabisa baada ya Aston Villa kuwapokeza kichapo cha 2-1 katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uliowakutanisha ugani Goodison Park mnamo Jumamosi.

Anwar El Ghazi alifungia Villa bao la ushindi katika dakika ya 80 na kudidimiza matumaini finyu ya Everton kukamilisha kampeni za EPL ndani ya mduara wa nne-bora muhula huu.

Ushindi huo wa Villa ulikuwa wao wa kwanza kusajili kutokana na jumla ya mechi 11 zilizopita ligini. Sasa ni jumla ya alama tisa ambazo zinawatanganisha Everton na Chelsea waliowapepeta Fulham 2-0 na kuingia ndani ya orodha ya nne-bora.

“Tulipoteza fursa nzuri ya kusalia kwenye vita vya kuingia nne-bora. Bado tuko kivumbini ila kwa sasa uwezekano ni mdogo zaidi na mtihani ni mgumu kabisa. Hatukuanza mechi dhidi ya Villa vizuri na hatukutarajia kwamba tungepoteza alama tatu kirahisi hivyo,” akasema Ancelotti.

Bao jingine la Villa lilifumwa wavuni na Ollie Watkins katika dakika ya 19, sita baada ya Everton kuwekwa kifua mbele na Dominic Calvert-Lewin. Watkins kwa sasa anajivunia jumla ya magoli 13 katika EPL msimu huu.

Everton almaarufu ‘The Toffees’ sasa wamejizolea alama 19 pekee kutokana na mechi 17 za nyumbani huku wakipoteza jumla ya michuano minane kati ya hiyo.

Baada ya kuwapepeta Arsenal katika mchuano wao wa awali, ilitarajiwa kwamba Everton wangaliwacharaza Villa kirahisi na kuweka matumaini ya kushiriki kivumbi cha UEFA msimu ujao.

Everton wamepangiwa kuvaana na West Ham United mnamo Mei 9, 2021 huku Villa wakiwaalika Manchester United ugani Villa Park.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Inter Milan sasa waweka mkono mmoja kwenye taji la Serie A

Atletico wacharaza Elche na kunusia ubingwa wa La Liga