• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 1:15 PM
Hatua ya Waiguru kutimua madaktari yamtatiza

Hatua ya Waiguru kutimua madaktari yamtatiza

GEORGE MUNENE na IRENE MUGO

Uamuzi wa Gavana Anne Waiguru wa Kirinyaga kuwafuta kazi madaktari na wauguzi mnamo 2019 umerudi kuathiri serikali yake baada ya Tume ya Huduma za Umma (PSC) kuiamuru iwarejeshe kazini na iwalipe malimbikizi ya mishahara yao ya miaka miwili.

Wahudumu hao wa afya waligoma wakilalamikia mishahara duni na mazingira mabaya ya kufanyia kazi.Kwa muda wa mwezi mmoja, madaktari na wauguzi walifanya maandamano mjini Kerugoya.

Serikali ya Gavana Anne Waiguru ilijibu kwa kuwapiga kalamu wahudumu hao ikiwalaumu kwa kuhujumu utawala wake.Wauguzi 188 walikata rufaa kwa Tume ya Huduma za Umma (PSC) ambayo iliwaondolea lawama na kuagiza serikali ya kaunti iwarejeshe kazini.

Katika uamuzi uliotolewa mnamo Machi 3, PSC ilitupilia mbali adhabu dhidi ya wauguzi hao ikiitaja kama iliyotolewa kinyume cha sheria.

Kulingana na barua ambayo tume hiyo ilituma kwa Bodi ya Utumishi wa Umma ya Kaunti (CPSB), PSC iliamuru serikali ya kaunti ya Kirinyaga itekeleze agizo hilo mara moja.

Lakini Gavana Waiguru alieleza kuwa nafasi za wauguzi hao 188 zilichukuliwa na wengine walioajiriwa baada ya wao kugoma.Aliongeza kuwa wauguzi hao waliofutwa, wanaweza tu kutuma maombi ya kazi endapo nafasi zitapatikana.

“Tunapanga kupanua baadhi ya vituo vya afya katika kaunti hii na huenda tukahitaji wahudumu zaidi wa afya. Endapo tutatangaza nafasi, wauguzi hao waliofutwa wanaweza kutuma maombi,” Gavana Waiguru akaeleza.

Bodi ya Utumishi wa Umma kaunti ya Kirinyaga (CPSB) pia imeomba PSC kuweka kando uamuzi wake wa kuwarejesha kazi wauguzi hao 188.

You can share this post!

DCI yaonya wasichana dhidi ya walaghai mtandaoni

JAMVI: Bunge linavyotishia kuongeza masaibu ya mswada wa BBI