• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
DOMO KAYA: Mtakuja kupigwa kiboko!

DOMO KAYA: Mtakuja kupigwa kiboko!

Na MWANAMIPASHO

LAZIMA mtakuwa mmesikia ile stori ya yule mwanamuziki wa injili Mr Seed aliyeamua kupanda mbegu kwenye shamba la wenyewe.

Unaambiwa bwana kapanda mbegu kwa mwanadada kwa jina Sabrina. Toka alipopanda mbegu, amegeuka mswahili. Mzee baba hayupo tayari kupokea mazao ya kazi yake.

Amekuwa akihangaika kushoto kulia kumshawishi Sabrina atoe mimba hiyo.

Binti wa watu alishajaribu mara mbili kufanya hivyo kwa kumeza vidonge fulani fulani na nusura akutane na Muumba wake kabla ya siku zake. Sababu iliyomfikisha hapo ni hofu ya nini atakachomwambia mamake. Hata baada ya kuepuka kifo bado mzee mbegu amekuwa akimshinikiza.

Binti wa watu kufanya la busara na kugoma. Kaaamua sasa kama mbaya acha iwe mbaya, lazima atamleta kiumbe huyo duniani. Hali hiyo imemwacha pabaya Mr Seed ambaye ana mke mzuri tu kwa jina Nimoh. Lile ndilo shamba lake halali. Sasa stori iliyopo ni kuwa mkewe baada ya kuzijua taarifa zile, kaamua kufungasha vyake ajitoe. Sio mara ya kwanza mzee wake kumweka katika hali kama hii.

Wakati skendo hii inachipuka, Mr Seed alikurupuka na kuachia wimbo mpya Ndoa, ngoma ya kimapenzi vile aliyomshirikisha swahiba wangu Kate Actress. Kuna walioamini kuwa sakata ile ilikuwa kiki tu ili kuisukuma kazi hiyo. Ila ukweli wa mambo ni kuwa jamaa alikurupuka kuachia ngoma hiyo ili ajaribu kutuliza makali ya skendo yake ya uhanyaji.

Napenda maelezo aliyoyatoa Kate kwamba hakujua kuna sakata kama hiyo na kamwe hawezi kujihusisha na kiki kutokana na kuwa brandi yake ni kubwa na wala hahitaji upuzi kama huo. Lakini kubwa hata zaidi, alisema hawezi kutumia masaibu ya mwanamke mwenzake kujifagilia. Labda niseme tu anaelewa vizuri maana ya kutokwa. Alipata ujauzito wake wa kwanza akiwa na umri wa miaka 19 na jamaa alimruka. Anaelewa machungu anayopitia Sabrina. Kate alisisitiza kuwa yeye ni kazi tu ndio aliyokuwa anatekeleza kwa mujibu wa makubaliano aliokuwa nayo na Mr Seed.

Hoja yangu ipo wapi? Hoja yangu ipo hapa. Hawa wasanii wa injili tulionao hasa wanaojifanya kuwa wa kizazi kipya wote ni ovyo. Hawa ndio wanaokemewa na Biblia kuwa wamevalia ngozi ya kondoo. Kazi yao ni uasherati huku wakitumia jina la Mungu kuficha maovu yao. Walishaoza zamani. Hawana la mno. Kheri kabisa wangefanya muziki wa ‘secular’ na skendo kama hizi ziwafuate. Sio kujifanya watakatifu wakati ni ovyo.

Niambie hata msanii mmoja wa injili wa kizazi kipya unayaweza kumlinganisha na Goodluck yule wa Tanzania? Huyo tu ndiye msanii wa injili wa kizazi kipya ninayemwona kuwa mkweli. Anagalu matendo yake yanaendana na imani yake.

Huyu Mr Seed pamoja na kuwa ‘mwinjilisti’ na mke bado tu alimfuata Sabrina. Jamaa alijigamba kuwa ana uwezo wa kuwatunza wanawake wawili. Maji yalipofika shingoni, jamaa akawa hana namna.

Huyu ni jamaa ambaye wakati alikuwa akimpagawisha binti wa watu, alikuwa anakosa hata fedha za kukodi chumba hotelini wafanye yao. Mtoto wa watu alipata ujauzito kwenye nyumba ya rafiki yake Mr Seed, msanii mwenzake Mash Mwana.

Huna uwezo wa kukodisha chumba ufurahie tunda la wizi ila unamwaminishia binti mdogo kuwa una uwezo wa kumtunza yeye pamoja na mke wako? Halafu kesho unaamka kwenda kuimba nyimbo za kumsifu Mungu. Hivi umerogwa nini? Unaogopa majukumu ya kulea. Hujali maisha ya binti wa watu. Basi kwa nini usingeusitiri mkia wako ndani ya suruali kama hukutaka kuchomewa picha? Mbona akili ndogo kama za ngiri mdogo wangu?

Sabrina alipokushtaki kwa pasta wako, ukadai kuwa huyo pasta ni ovyo. Acheni kiburi kwa jina la Mungu. Mtakuja kupigwa viboko nyie. Hapa nilipo namwombea dua Sabrina. Nimemwona ni binti mchanga, aliyedanganywa na ule ustaa wa mzee mbegu, wakati jamaa hana lolote.

Namwombea ajaliwe huyo mtoto amlee kama awezavyo. Mzee mbegu acha nisubiri kuona hatua atakayoichukua Nimoh. Itakuwa vyema kama akiondoka ila kama jinsi mamangu husema kila siku, wawili waliojifunika shuka moja, usithubutu kuingilia ya kwao.

 

You can share this post!

KASHESHE: Walamba dili tamu

Machifu sasa kulipwa pesa za kuinua motisha