• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 2:25 PM
NASAHA ZA RAMADHAN: Si lazima watu kukesha msikitini wakati huu wa kafyu, swali nyumbani

NASAHA ZA RAMADHAN: Si lazima watu kukesha msikitini wakati huu wa kafyu, swali nyumbani

Na SHEIKH MOHAMED KHALIFA

TUMSHUKURU Mwenyezi Mungu (SWT) kutufikisha Ijumaa ya mwisho ndani ya mwezi huu wa Ramadhani.

Alhamisi tulizungumza kuhusu usiku wa Laylatul Qadir na jinsi ya kuupata. Mojawapo ya mambo yanayosisitizwa ni kuhamia msikitini kwa siku kumi za mwisho. Kitendo hiki cha kwenda msikitini huitwa Itikaf.

Lakini safari hii, kama ilivyokuwa mwaka jana, usiku hakuna kutoka nje sababu ya kafyu. Ikiwa mtu aliingia na anaendelea kubaki ndani ya msikiti, hiyo ni sawa.

Hivyo, swala ya Tahajjud, ambayo kwamba ni sunna (mwenendo wa Mtume Muhammad), kwa sasa haiwezekani.

Vile vile, watu hawawezi kuswali bega kwa bega kama ilivyo kanuni ya kupanga swafu misikitini.

Jambo muhimu katika Uislamu ni watu kumuabudu Mwenyezi Mungu (SWT) kwa njia ya wepesi.

Afanye alivyofanya mtume (SAW): aamshe familia yake na pamoja waswali hiyo swala ya Tahajjud ambayo hufanywa katika thuluthi ya mwisho ya usiku.

Anaweza kuwaamsha kuanzia saa nane na nusu au saa tisa hadi wakati wa kula daku, ambao huwa imeingia Fajir.

Hudheifa (R.A) alinukuliwa kwenye Sahih Bukhari akisema, “Kila Mtume (SAW) aliponyanyuka usiku kwa ajili ya Tahajjud, alikuwa akipiga mswaki.”

Naye Abdalla Bin Umar (R.A) alisema alikuja mtu kwa Bwana Mtume (SAW) akamuuliza, “Ewe Mtume, swala ya usiku inaswaliwaje?” Akasema, “Rakaa mbili na kutoa salamu, rakaa mbili tena kuendelea hadi utakapokaribia wakati wa kula daku (anapoadhini muadhini wa kwanza), swali rakaa moja ya witr.”

La muhimu ni kwamba Muislamu anaweza kutekeleza ibada nyakati za usiku hata kama ni ndani ya nyumba yake. Si lazima atoke kwenda msikitini iwapo hali hairuhusu.

Lakini pia kuwepo kwa kafyu kusiwe kisingizio kwa watu kuacha kuamka usiku na kutafuta fadhila ya Mwenyezi Mungu (SWT), hasa ndani ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Ndugu msomaji, usipoteze fursa hii kubwa ya kuwa miongoni mwa watakovuna mema mengi, kama alivyotuahidi Mwenyezi Mungu (SWT) na Mtume wake.

You can share this post!

Kenya yachukua ubingwa katika soko la mihadarati

Hofu safari zikikwama Mto Athi sababu ya mamba